Mradi wa Reproductive Equity Strategy in Tanzania (REST), unaotekelezwa na shirika la DSW Tanzania kwa kushirikiana na shirika la Alama Yangu na Tahea, umeingia katika vyuo vikuu vya mkoani Iringa kuwasaidia vijana wa vyuo vikuu kukabiliana na changamoto ya ukatili wa kijinsia na afya ya uzazi.
Mahusiano ya kimapenzi miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Iringa yameelezwa kuwa moja ya vyanzo vikuu vya ukatili wa kijinsia unaowakumba wanafunzi wa kike.
Vyuo vikuu vilivyolengwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCo), na Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI).
Mbali na ukatili wa kijinsia na afya ya uzazi, Mkurugenzi wa DSW, Peter Owaga alisema mradi huo utazingatia pia kuimarisha elimu kuhusu afya ya akili, madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, stadi za maisha, na kutoa mafunzo maalum yanayohusu usawa wa kijinsia.
REST pia itahamasisha uanzishwaji wa klabu za afya vyuoni ambazo zitakuwa majukwaa ya kutoa msaada wa kisaikolojia, kuhamasisha taarifa za ukatili, na kujenga mtazamo mpya wa usawa wa kijinsia miongoni mwa wanafunzi huku ukiwa na lengo la kuwasaidia vijana kujitegemea kiuchumi na kijamii.
Katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Sunset mjini Iringa kuelezea malengo ya mradi huo, Owaga alisema mradi wa REST utawahusisha vijana walioko ndani na nje ya mfumo rasmi wa elimu, kutokana na changamoto nyingi zinazowakumba.
Kaimu Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Iringa, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Lidya Sospeter, alisema kuwa mahusiano ya kimapenzi vyuoni mara nyingi husababisha migogoro ambayo huishia kuwa ukatili wa kijinsia.
“Mahusiano haya mara nyingi yanajumuisha udhalilishaji wa kingono, shinikizo la kihisia, au hata matumizi ya nguvu. Wanafunzi wengi wa kike wanajikuta wakikubali mahusiano yasiyofaa kutokana na utegemezi wa kifedha au hofu ya unyanyapaa,” alisema Sospeter.
Aidha, alibainisha kuwa matukio ya ukatili hayaripotiwi kwa sababu ya woga au aibu, jambo linalochochea kuendelea kwa changamoto hii.
“Kupitia mradi wa REST, tunalenga kutoa elimu itakayosaidia kuwahamasisha wanafunzi wa vyuo vikuu kuripoti matukio haya na kuimarisha usawa wa kijinsia,” aliongeza.
Mwenyekiti wa Waelimisharika kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Soni Moses John, alisema kuwa ukatili wa kijinsia unaanzia kwenye fikra potofu kwamba mwanaume ndiye mwenye mamlaka makubwa katika uhusiano.
“Suala la mahusiano vyuoni limekuwa sababu kuu ya ukatili. Migogoro huibuka pale ambapo mmoja wa wahusika anapojaribu kudai mamlaka, na hatimaye migogoro hii hupelekea vipigo au unyanyasaji wa kihisia,” alisema.
Kwa upande wake, Amina Msangi, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, alieleza kuwa baadhi ya wanafunzi wa kike wanaogopa kutoa taarifa za ukatili kwa hofu ya unyanyapaa.
“Kuna wakati unalazimishwa kufanya jambo kinyume na mapenzi yako, lakini unaamua kunyamaza ili kulinda heshima yako au kuepuka lawama. Lakini huu ni wakati wa mabadiliko, lazima tuwe na ujasiri wa kuripoti matukio ya ukatili,” alisema Amina.
Mratibu wa Mradi wa REST, Selina Protas, alieleza kuwa mradi huu utatekelezwa katika kata za Ifunda, Mseke, Kising’a, na Kihorogota kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, pamoja na kata za Ruaha, Makorongoni, Mkwawa, Kihesa, na Mtwivilla kwa Manispaa ya Iringa.
“Tutaanzisha Klabu za Afya vyuoni zitakazoongozwa na vijana vinara ‘champions’ waliopatiwa mafunzo maalum. Klabu hizi zitakuwa vituo vya maarifa, usaidizi, na mazungumzo ya mabadiliko,” alisema Protas.
Alisema mradi pia utashawishi na kuchochea mafunzo ya stadi za maisha yatakayowasaidia vijana kufanya maamuzi sahihi, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, na kujenga uhusiano wenye afya.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Iringa, Fatuma Mohamed, alisema kuwa elimu itakayopatikana kupitia REST itakuwa chachu ya mabadiliko miongoni mwa vijana.
Meneja wa mradi wa REST kutoka shirika la Alama Yangu, Joyce Ernest alisema matarajio yao katika utekelezaji wa mradi huo ni wadau wao wote wapata uelewa wa kutosha kuhusu afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia.
“Kwa vijana tunataka wajisemee vizuri sana juu yale yanayowakabili kuhusu afya ya uzazi na ukatili, ili watoa maamuzi waweze kuwasikia na waweze kufanya maamuzi sahihi katika kuimarisha mifumo na utekelezaji wa sera ili wapate huduma stahiki,” alisema.