Mraid wa bil 1.3/-waongeza uzalishaji maji safi Bukombe

GEITA: WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Bukombe mkoani Geita imekamilisha utekelezaji wa mradi wa maji Mwalo-Nakayenze wenye thamani ya Sh bilioni 1.3 na uwezo wa kuzalisha takribani lita 150,000.
Mradi huo wa maji wa Mwalo-Nakayenze upo katika maeneo mawili ambapo kwa upande wa kijiji cha Mwalo umehusisha ujenzi wa tenki la ujazo wa lita 75,000 na upande wa Nakayenze pia kuna tenki la lita 75,000.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Bukombe, Mhandisi James Benny ametoa taarifa hiyo kwa viongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2025 katika uzinduzi wa mradi huo kijiji cha Mwalo kata ya Ushirombo.

Amesema upande wa Mwalo mradi umehusisha ulazaji wa mabomba km 15.7 na vituo saba vya kuchotea maji ambapo chanzo cha maji katika mradi huo ni kisima kirefu cha mita 100 chenye uwezo wa kutoa lita 5,000 kwa saa.
“Kwa upande wa kijiji cha Nakayenze kata ya Busonzo mradi umehusisha ujenzi wa jengo la nishati, tenki la ujazo wa lita 5,000 huku chanzo cha mradi ni kisima kirefu cha mita 100 chenye uwezo wa kuzalisha lita 6,000 kwa saa” amesema.
Amesema mradi ulianza kutekelezwa Desemba 2023 na kukamilika Desemba 2024 chini ya mkandarasi M/S D4N Co.Ltd wa Kahama ambapo mpaka sasa.

Mhandisi Benny amesema miradi hiyo imeboresha na kusogeza huduma ya maji safi na salama na kupunguza muda wa kufuata maji umbali mrefu na kuongeza kiwango cha huduma ya maji safi kufikia asilimia 63.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Mwaka 2025, Ismail Ali Ussi amesema kukamilika mradi ni hatua ya kwanza kuelekea hatua inayofuata ya uboreshaji wa huduma ya maji ambayo inategemea uendelezaji wa miradi.

Ussi amesema dhamira ya serikali ni kuona huduma ya maji safi na salama inakamilika kwa asilimia 100 kwenye vijiji vyote nchini na hivo kila mradi unapaswa kutekelezwa, kukamilishwa na kuendelezwa kwa kiwango sahihi.



