Mratibu THRDC awafunda vijana wa vyuo

DAR ES SALAAM: Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, amewataka vijana walioko katika vyuo vya juu kutumia muda wao kwa mambo yenye manufaa na kuanza kujaribu kutekeleza ndoto zao kabla ya kuhitimu masomo.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa uzinduzi wa kitabu kipya cha “Watanzania na Sheria,” kilichoandikwa na mwanafunzi wa Shule Kuu ya Sheria, Onesmo Mathew Daud, ambaye pia ni mtetezi wa haki za binadamu.

Akizungumza kuhusu hatua ya kijana huyo, Wakili Olengurumwa amesema kuandika kitabu akiwa bado mwanafunzi ni ushuhuda wa wazi kuwa elimu ya chuo kikuu si kikwazo cha mtu kuanza kutekeleza malengo yake ya baadaye.

“Pamoja na kuwa Onesmo Mathew bado ni mwanafunzi, tayari ameandika kitabu chake cha kwanza ‘Falsafa za Haki za Binadamu’ na sasa hiki cha pili. Hii ni ishara kwa wanafunzi kwamba chuo ni sehemu ya maandalizi ya maisha na ni muhimu kuanza kujaribu kile utakachokiishi baada ya kuhitimu,” amesema.

Aidha, amempongeza Mathew kwa hatua hiyo na kusema ni mwanzo mzuri wa safari yake ya kuwa mwandishi bora wa vitabu vinavyoelimisha jamii kuhusu masuala muhimu.

Kwa upande wake, mwandishi wa kitabu hicho, Onesmo Mathew, amesema kuwa “Watanzania na Sheria” kimeandikwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi kuelewa masuala ya kisheria yanayowakabili katika maisha yao ya kila siku na kujua haki pamoja na wajibu wao.

Mathew pia amewaomba Watanzania kuunga mkoni juhudi za kijana huyo kujipatia nakala ya kitabu hicho kwa kupiga simu nambari +255 715 051 792.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button