Msajili ahoji maelezo ugombea wa Mpina

DAR-ES-SALAAM : OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekiandikia barua Chama cha ACT Wazalendo kikitaka maelezo kuhusiana na malalamiko yaliyowasilishwa na mwanachama wake, Monalisa Ndala, anayepinga uteuzi wa Luhaga Mpina kugombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho.

Monalisa, ambaye ni Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, aliwasilisha malalamiko kwa Msajili akidai chama chake kimekiuka sheria na kanuni za ndani katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais.

Akizungumza na HabariLEO jana, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alithibitisha kupokea barua ya malalamiko hayo. “Ni kweli tumepokea barua kutoka kwa mwanachama wa ACT Wazalendo, Monalisa Ndala, akipinga uteuzi wa mgombea urais wa chama hicho kwa madai kuwa haukufuata sheria na kanuni za chama. Tumeshawandikia ACT Wazalendo barua ya kuwataka watupatie maelezo na tumewapa muda hadi kesho (leo),” alisema Nyahoza.

Taarifa zinaeleza kuwa Agosti 14, mwaka huu, siku moja kabla ya Mpina kuchukua fomu katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Monalisa aliwasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa chama hicho akipinga hatua ya kumteua. SOMA: Mpina aenguliwa kugombea urais

Juzi, akizungumza kupitia kipindi cha Clouds 360, Monalisa alidai kuwa mchakato wa kumteua Mpina ulikiuka baadhi ya kanuni za chama, ikiwamo sharti la mgombea kuwa mwanachama wa ACT Wazalendo si chini ya mwezi mmoja kabla ya mwisho wa uteuzi.

Alisema pia mgombea anatakiwa kuwa mtu anayeielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za chama na kuonesha utayari wa kuishi kwa misingi hiyo. “Wakati chama kinatangaza mchakato wa ndani Aprili 18, 2025, Mpina alikuwa bado CCM. Ili kukidhi vigezo, alipaswa kujiunga mapema Januari, Februari au Machi,” alisema Monalisa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button