Msako nyumba kwa nyumba watoto wasioripoti shuleni

DIWANI wa Kata ya Nyanguku Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Elias Ngole ametangaza kufanyika kwa operesheni maalumu kwa ajili ya kusaka watoto ambao hawajaripoti shule. Operesheni hiyo inatarajiwa kuanza Januari 19, 2026 kwa kushirikisha askari wa sungusungu watakaopita kila nyumba kusaka wanafunzi wa awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza.

Ngole ametangaza operesheni hiyo jana mbele ya wazazi na walimu katika hafla ya kugawa madaftari kwa wanafunzi wote wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Nyanguku. SOMA: Nyang’hwale mguu sawa kupokea kidato cha kwanza

Amesema hatua hiyo inalenga kuunga mkono serikali kuhakikisha kila mtoto mwenye sifa ya kuanza masomo kwa shule za msingi na sekondari aweze kupata haki hiyo pasipo kikwazo. “Kama una mtoto alitakiwa kuanza chekechea, darasa la kwanza umekaa naye nyumbani, tutakuja kwako. Kama umekaa na mtoto hajaripoti shule, Jumatatu tunakuja kwako,” alisema.

Amesema ajenda ya kugawa madaftari kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza wa kata hiyo ni endelevu na kwa sasa imefikia miaka mitatu, dhamira ikiwa kuhamasisha watoto kwenda shule. Ngole amesema mbali na kugawa madaftari kila mwaka, tathmini inapaswa kufanyika kila mwaka juu ya mwitikio wa wanafunzi kuendelea na elimu ya sekondari pamoja na ufaulu wa wanafunzi.

Ofisa Elimu Kata ya Nyanguku, Innocent Yasasa amesema kata hiyo ina shule za sekondari mbili ambazo ni Nyanguku na Nyakato-Geita zinazotarajia kupokea wanafunzi 204 kidato cha kwanza. Amesema Shule ya Sekondari Nyanguku wamesharipoti wanafunzi 90 kati ya 135 sawa na asilimia 66, huku Shule ya Sekondari Nyakato wameripoti wanafunzi 39 kati 69 sawa na asilimia 56.

Yasasa amesema kwa madarasa ya awali, wameshapokea wanafunzi 151 kati ya 300 sawa na asilimia 50, huku kwa darasa la kwanza wameripoti watoto 301 kati ya 576 sawa na asilimia 50.3.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button