MSF ipo tayari mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko

SHIRIKA la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limetangaza kuwa lipo tayari kushirikiana na Wizara ya Afya ya Tanzania kwa kutoa msaada zaidi katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko iwapo litaombwa kufanya hivyo.
Taarifa hiyo imetolewa leo Machi 14, 2025, na Mkuu wa MSF-Tanzania, Tommaso Santo kufuatia tangazo rasmi la Tanzania kuwa haina tena mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg.
Tangazo hilo limekuja baada ya siku 42 kupita bila kuripotiwa kwa kesi mpya. Mlipuko huo uliathiri Mkoa wa Kagera, ambapo ulisababisha kesi za ugonjwa huo na vifo kadhaa.
Katika kukabiliana na mlipuko huo, MSF ilishirikiana na Wizara ya Afya kwa kutuma timu yenye uzoefu ili kusaidia juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.
Shirika hilo lilitoa mafunzo kwa wahudumu wa afya katika zaidi ya vituo 30 vya kutolea huduma, kuboresha miundombinu ya vitengo vya kutenga wagonjwa, na kuanzisha maeneo maalum ya kuvalia na kuvua vifaa vya kujikinga. Pia, waliboresha vituo vya kufulia ili kuhakikisha usafi na uondoshaji salama wa uchafu kutoka kwenye mavazi ya kujikinga na vifaa vya afya.
Akizungumzia mchango wa shirika hilo, Tommaso Santo amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, MSF limeisaidia Tanzania kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, surua na Marburg.
“Tunajitahidi kuwa mshirika wa matibabu anayeaminika, si tu katika kukabiliana na milipuko ya dharura, bali pia katika majanga ya asili na magonjwa mengine ya mlipuko,” amesema Santo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Matibabu cha Dharura cha Marburg Biharamuro, Dk. Michael Kiremeji, amesifu mchango wa MSF, ambapo amesema kuwa shirika hilo ni msaada mkubwa hasa katika nyakati za dharura, huku akiongeza kuwa iwapo kutatokea dharura nyingine, watahakikisha msaada unapatikana na wagonjwa wanapata matibabu sahihi kwa wakati muafaka.
Aidha, MSF imeeleza kuwa itaendelea kuongeza uelewa wa umma kuhusu Homa za Virusi Zinazosababisha Kutokwa na Damu (VHFs) kwa kuimarisha hatua za kinga kupitia mipango maalum ya kufikia jamii, ushirikishwaji wa wananchi, na kampeni za elimu ya afya.



