Mshikamano wahitajika mageuzi kiuchumi

ARUSHA: Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Hashil Abdallah amesema ili kufanikisha mageuzi ya kiuchumi na teknolojia kunahitajika mshikamano thabiti kati ya waajiri na wafanyakazi kwa misingi ya kuheshimiana, kushirikiana na kutimiza wajibu kila upande.

Hashil amesema hayo leo Septemba 19, katika ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi Taifa la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na kudai wakala huo una mchango mkubwa katika kujenga uchumi imara na kutokana na hali hiyo menejimenti ya taasisi hiyo inapaswa kuendelea kuimarisha mifumo ya kidigitali na kuongeza uwazi na uwajibikaji na kwa gharama nafuu.

Amesema hatua hiyo itaongeza imani kwa wananchi na wawekezaji na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika jitihada za serikali za kukuza uchumi na uwekezaji nchini.

Amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi ikiwemo upungufu wa vitendea kazi,shinikizo la kazi nyingi, na wakati mwingine ucheleweshaji wa baadhi ya maslahi, Wizara ya ya Viwanda na Biashara itaendelea kushirikiana kwa karibu na Brela kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Katibu Mkuu aliwataka wajumbe wa kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi Brela kupitia na kujadili taarifa ya utendaji ya Wakala kwa mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa mipango mkakati wa Wakala 2021/22 hadi 2025/26 kwa kipindi cha miaka minne.

Amesema hiyo ni hatua muhimu kwani inatoa fursa ya kutathmini utekelezaji wa majukumu ya Wakala,kufahamu mafanikio yaliyopatikana,changamoto zilizojitokeza na kuja na mikakati madhubuti ya kuimarisha zaidi utendaji wake wa miaka ijayo.

Katibu Mkuu huyo aliendelea kusema kuwa kikao hicho kitajadili pia taarifa ya mapitio ya mpango wa motisha wa wakala pamoja na na kanuni za utumishi za Wakala Brela Staff Regulations ,majadiliano hayo ni muhimu kwani yanahusu moja kwa moja masuala ya ustawi wa watumishi, motisha zao na mwongozo wa namna bora ya kuendesha kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya watumishi.

Amesema mapendekezo hayo yatatokana na mjadala wa kuimarisha zaidi nidhamu,uwajibikaji na ari ya watumishi katika utekelezaji majukumu ya kila siku yenye lengo la kuijenga na kuimarisha Brela ili iweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake kwa maslahi ya taasisi na nchi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushari Brela, Professa Neema Mori kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi aliwataka wafanyakazi wa taasisi hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamno wenye lengo la kuongeza ufanisi na mafanikio kwa taasi hiyo.

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa amesema kuwa baraza hilo ni la kwanza kwa mwaka huu wa fedha na litajadili na kufanya maamuzi kuhusu agenda tatu ikiwa ni pamoja na kujadili na kupitia utekelezaji wa bajeti mwaka 2024/25,kupata mrejesho kuhusu utekelezaji wa kipindi cha miaka minne yaani 2021/22-2025/26 na kupitia taarifa ya mapitio ya mpango wa motisha wa Wakala ‘Brela Incentive Scheme’ pamoja na kanuni za utumishi za wakala ‘Brela Staff Regulations’.

Nyaisa alisema kwa mwaka huu wa fedha 2024/25,Wakala imefanikiwa kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa kufikia zaidi ya silimia 115 ya lengo lililowekwa vilevile wameendelea kuboresha utoaji wa huduma za sajili na leseni mbalimbali ambapo kwa wstani wamefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 110 ya malengo yao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button