Mshindi Tamasha la Mavazi Samia akabidhiwa mil 3/-

MWANAMITINDO wa Kimataifa Millen Happiness Magese amekabidhi hundi yenye thamani ya Sh milioni tatu kwa mwanamitindo Elizabeth Masuka aliyeibuka mshindi wa Samia Fashion Festival Zanzibar mwaka 2024.

Magese aliyekuwa Jaji Mkuu wa Samia Fashion Festival Zanzibar alikabidhi hundi hiyo Dar es Salaam katika hafla fupi baina yao akisema fedha hizo zimetoka Kampuni ya Millen Prive & Co Lifestyle ambayo yeye ndio Mkurugenzi Mkuu.
Amesema anatambua mchango mkubwa unaofanywa na wanamitindo hivyo, kuwamua kuwatia moyo wale wenye jitihada akiwemo Elizabeth.

“Tunafahamu kulikuwa na Samia Fashion Festival Zanzibar ambalo liliandaliwa na dada yangu Khadija Mwanamboka na katika tukio hilo nilikuwa Jaji Mkuu ,hivyo baada ya kutangaza washindi niliona umuhimu wa kuitambua kazi kubwa iliyofanywa na wanamitindo walioshiriki usiku huo,”

Advertisement

 


Amesema amefurahishwa kufanyika kwa Samia Fashion Festival Zanzibar kwani limethibitisha nafasi na umuhimu wa wanamitindo nchini Tanzania lakini pia kutoa nafasi ya vijana wa Kitanzania kuonesha uwezo wao katika kutawala Jukwaa la wanamitindo.

Magese amesema anajivunia kushuhudia wanamitindo wote walioshiriki na kuonesha uwezo wao huku akisisitiza kwa zaidi ya miaka ishirini amejitolea maisha yake katika sekta ya mitindo na urembo.

Amesema mitindo inathaminika zaidi katika nchi za Ulaya na mataifa mengine, si tu kama sanaa bali kama alama ya utambulisho, urithi, na fahari na kutoa rai kwa Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau pamoja na Serikali chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kuinua na kuendeleza sekta ya utamaduni,mitindo na urembo.

Kwa upande wake mwanamitindo Elizabeth amesema kukutana kwa mara ya kwanza na Millen ilikuwa ni ndoto iliyotimia na amefurahi kumuona ana kwa ana na kwa jinsi alivyo na mafanikio.

“Nimejifuza kitu kipya kutoka kwake, zawadi ambayo alinipa ilikuwa furaha yangu ya pili baada ya kazi nzuri ambayo imefanyika, namshuru sana na kumuombea Mungu aendelee kumuweka kwa ajili yetu, ni mtu mwema sana, kutoka kwake niliona mtu ambaye anataka kuona wanamitindo wengine nchini Tanzania wakifanikiwa,”amesema.