“Msiingilie daftari la kudumu la mpiga kura”

VIONGOZI wa vyama mbalimbali vya siasa wametakiwa kutoingilia mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura katika vituo vya uandikishaji wa daftari hilo badala yake vitate sheria, taratibu na kanuni husika.

Akizungumza leo mkoani mtwara wakati wa mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2025, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema vyama hivyo ni vema vikatumia taratibu zilizoainishwa katika sheria zinazosimamia uchaguzi.

Mkutano huo umefanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani lengo likiwa ni kutoa elimu ya mpiga kura ili kuhakikisha wadau wote wanapata fursa ya kuelimika na kuelewa mchakato huo.

Pia wafate maelekezo ya tume na kusimamia miiko na mipaka ya uendelezaji wa zoezi la uboreshaji wa daftari hilo.

“Tume kwa upande wetu tutazingatia Katiba ya uchaguzi na kanuni zilizotungwa chini ya sheria katika zoezi hili la uboreshaji”amesema Mwambegele.

Amesema, zoezi hilo haliwahusu wapiga kura wenye kadi hizo za kupigia kura na ambao kadi zao hazijaharibika, kupotea au hawajahama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo jingine au taarifa zao hazijakosewa hivyo hawahitaji kuboresha taarifa zao.

Zoezi hilo la uboreshaji linafanyika kwa muda wa siku saba ambapo kwa Mkoa wa Mtwara zoezi kitaanza Januari 28, 2025 hadi Februari 3, mwaka huu.

Kwa Upande wa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhani amesema mkoa huo unatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 17,719 ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 930,840 waliyopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Hata hivyo tume hiyo inatarajia baada ya uandikishaji mkoa huo utakuwa na wpiga kura 1,056,814.

Pia jumla ya vituo 1,806 vitatumika kwenye uboreshaji huo kwa mwaka 2025 ikiwa ni ongezeko la vituo 30 katika vituo 1,776 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.

Mjumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi, Dk Zakia Abubakar ametoa rai kwa wadau wa Mkutano huo kuendelea kuwahamasisha wananchi mkoani humo kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo la uboreshaji.

Ushiriki huo wa wananchi katika zoezi hilo itapelekea kuwa na sifa ya kuchagua viongozi mbalimbali kwa nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button