Mtwa Adam Sapi II aamsha Uhehe, Kalenga kufurika Hehe Day 2025

IRINGA: KATIKA juhudi za kuenzi urithi wa Mtwa Mkwawa kama shujaa na mwanzilishi wa Uhehe wa sasa, na kukuza ushujaa wa kihehe katika nyanja za kijamii na kiuchumi, Chifu wa Wahehe, Mtwa Adam Sapi II, ametangaza rasmi maadhimisho ya Hehe Day 2025.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika kijijini kwa chifu huyo, Kalenga – wilayani Iringa – kuanzia Juni 17 hadi 19, mwaka huu.
Ni tukio linalotazamwa kuwa na uzito mkubwa katika historia ya utamaduni wa kihehe na ustawi wa jamii kwa ujumla.
“Maadhimisho haya si tu ni kumbukumbu ya mashujaa wetu waliopigana kwa ujasiri kulinda uhuru na utamaduni wa Kihehe dhidi ya ukoloni wa Kijerumani, bali pia ni jukwaa muhimu la kujenga mshikamano wa kijamii,” alisema Mtwa Adam Sapi II akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa.
Amesisitiza kuwa maadhimisho haya yanabeba dhamira ya kuhamasisha maendeleo endelevu, sambamba na kuitafsiri mila na desturi za Kihehe kama msingi wa maendeleo ya jamii na taifa.
“Tunalo jukumu la kukijengea ari kizazi cha sasa na kijacho kuelewa na kuthamini historia yao. Urithi huu wa mashujaa wetu ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya jamii yetu,” aliongeza.
Kwa mujibu wa ratiba ya matukio, siku tatu za maadhimisho hayo zitajumuisha matambiko ya kimila na maombi ya heshima kwa mashujaa waliotangulia, na ziara katika maeneo ya kihistoria kama Kalenga na Lugalo ili kukuza utalii wa kiutamaduni.
Aidha alisema kutakuwa na maonesho ya bidhaa mbalimbali – za jadi na kisasa – pamoja na utoaji wa tuzo kwa watu na taasisi zilizojitokeza kuenzi na kulinda urithi wa Kihehe.
Lakini pia kutakuwa na mijadala na makongamano ya kitaaluma yatakayogusia mchango wa urithi wa kihistoria katika maendeleo ya sasa, sambamba na ushiriki wa vijana, wanawake na wazee.
Mwenyekiti wa Mkwawa Foundation inayoratibu maadhimisho hayo, Omary Mahinya Mkwawa, amesema ndoto yao ni kuhakikisha Hehe Day inapata hadhi ya kitaifa na inakuwa sehemu rasmi ya kalenda ya matukio ya kiutamaduni nchini Tanzania.
“Tunaamini tukio hili lina nguvu ya kuunganisha historia na mustakabali wa jamii yetu. Ni wakati wa kutazama tamaduni zetu kama rasilimali muhimu ya maendeleo,” alisema.
Akitaja malengo ya Hehe Day 2025, Mahinya alisema yanaenda mbali zaidi ya kumbukumbu; yanalenga kuelimisha jamii kuhusu historia ya Kihehe, kuimarisha maendeleo endelevu kupitia utalii wa kiutamaduni, kuibua fikra mpya za maendeleo, na kulinda utambulisho wa Wahehe kwa vizazi vijavyo.
Maadhimisho ya mwaka huu alisema yamebeba kaulimbiu isemayo: “Utamaduni Wetu, Urithi Wetu.”
Alisema kaulimbiu hiyo inaakisi dhamira ya kuunganisha historia, mila, na maendeleo ya kisasa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



