MBEYA; JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia mume na mke kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wao, Chloy Ramadhan (4) kwa kumpiga na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kosa la kujisaidia kwenye nguo.
Tukio hilo ni la juzi saa 2 usiku katika Mtaa wa Teku viwandani baada ya baba mzazi wa mtoto huyo, Ramadhan Mwakilasa (28) akishirikiana na mama wa mtoto wa kambo, Mariamu Mwashambwa (28) kumpiga mtoto huyo na kisha kusababisha kifo chake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alisema uchunguzi umebaini tukio hilo ni ukatili na unyanyasaji wa kumuadhibu mtoto kwa kujisaidia kwenye nguo alizokuwa amezivaa.
Kamanda Kuzaga aliwataka wazazi na walezi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watoto pindi wanapokosea, badala yake watumie njia sahihi na salama kuwafundisha au kuwaelekeza bila kusababisha madhara.