Mutharika aongoza matokeo ya awali urais

MALAWI: RAIS wa zamani wa Malawi, Peter Mutharika, anaongoza katika uchaguzi uliofanyika Septemba 16, 2025, kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoka robo ya mabaraza ya nchi hiyo.
Mutharika amepata takribani asilimia 51 ya kura halali katika mabaraza tisa kati ya 36, huku Rais Lazarus Chakwera akipata karibu asilimia 39. Mgombea anahitaji zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kushinda moja kwa moja, vinginevyo duru ya pili itafanyika.
Wachambuzi wa siasa nchini humo walitabiri mapema kuwa uchaguzi huo ungelikuwa ni pambano kati ya Mutharika na Chakwera, ambao wamekuwa wakikabiliana mara kwa mara katika chaguzi za urais.
Malawi imeendelea kukumbwa na changamoto za kiuchumi chini ya utawala wa Chakwera, ikiwemo mfumuko wa bei uliozidi asilimia 20 kwa zaidi ya miaka mitatu, ukame na vimbunga vinavyohusishwa na mabadiliko ya tabianchi. SOMA: Uchaguzi Mkuu Malawi kufanyika leo
Mutharika, profesa wa sheria na rais wa Malawi kati ya mwaka 2014 na 2020, anasifika kwa kuboresha miundombinu na kupunguza mfumuko wa bei, ingawa anakumbukwa pia kwa tuhuma za upendeleo ambazo alikanusha.
Chakwera, mchungaji wa zamani mwenye umri wa miaka 70, aliingia madarakani mwaka 2020 baada ya Mahakama ya Katiba kufuta ushindi wa Mutharika katika uchaguzi wa 2019. Tume ya Uchaguzi imesema itatangaza matokeo kamili ifikapo Septemba 24 na imeonya wagombea kutokujitangazia ushindi kabla ya muda.