DAR ES SALAAM; MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam imemhukumu aliyekuwa Ofisa Tehama wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji Kampasi ya Dar es Salaam amlipe fidia Sh milioni 10 mwanafunzi aliyemuomba rushwa ya ngono.
Hakimu Mkazi Mkuu, Rehema Lyana alitoa hukumu hiyo katika shauri la uhujumu uchumi namba 16/2022.
Katika shauri hilo, Michael Msangawale alitiwa hatiani baada ya kufanya makubaliano ya maridhiano katika shauri dhidi yake.
Ofisa huyo alishitakiwa akidaiwa kutaka rushwa ya ngono kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, rejeo la mwaka 2019 ikisomwa pamoja na Jedwali la 21 la aya ya kwanza ya kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Kudhibiti Uhujumu Uchumi (EOCCA).
Ilidaiwa mahakani hapo kuwa mshitakiwa aligoma kumwekea matokeo katika mfumo mwanafunzi mmoja ili aweze kuendelea na masomo yake katika hatua ya stashahada kwa sharti la kupewa ngono.
Mshitakiwa aliomba kufanya majadiliano ya maridhiano wiki iliyopita, mahakama ikaridhia na kumtia hatiani baada ya kukiri kosa na kulipa fidia ya Sh milioni kumi ambazo atapatiwa mwanafunzi aliyetakiwa kutoa rushwa ya ngono.
Wakati huohuo Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Tunduru imewahukumu Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Nambalapi, Shaibu Basi Swala, Mwenyekiti wa kijiji cha Nambalapi, Shaibu Omary Shaibu na Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji, Shabani Tukuru Mohamedi kulipa faini ya Sh 800,000 kila mmoja au kwenda jela miaka minne.
Wametiwa hatiani kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, mapitio ya mwaka 2024.
Hukumu hiyo ilitolewa Novemba 25, 2024 na Hakimu Mkazi Wilaya ya Tunduru, Lilian Haule.
Washitakiwa walifikishwa mahakamani Novemba 7 mwaka huu wakidaiwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh 1.75 ili wamuuzie mkulima, Seleli Mwabila shamba.
Ilidaiwa kuwa walimuuzia kwa makusudi eneo la Msitu wa Hifadhi ya Kijiji cha Nambalapi, ekari 75 kinyume na sheria.
Washitakiwa walihukumiwa kulipa faini Sh 800,000 kila mmoja au kufungwa jela miaka minne. Walilipa faini.
Shauri liliendeshwa na waendesha mashitaka wa serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Havin Charles, Nuru Muyinga na Mwinyi Yahaya.