Mwanafunzi Veta aibuka mshindi kupika chapati

DAR ES SALAAM; MWANAFUNZI wa fani ya mapishi kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) Chang’ombe, Dar es Salaam, Neema Mwang’onda ameibuka mshindi wa kwanza kwenye mashindano ya kupika chapati yaliyowakutanisha mamalishe zaidi ya 250.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Kituo cha Televisheni cha EATV, yalifanyika juzi katika viwanja vya Mbagala Zakheem, Dar es Salaam.

Mwang’onda amejishindia Sh 600,000, jokofu, kiwanja na kujiendeleza kusomea fani hiyo katika Chuo cha Utalii Tanzania.

Advertisement

Akizungumza baada ya ushindi huo, Mwang’onda alisema kuwa sababu za kushiriki katika mashindano hayo ni kwa kuwa anapenda kupika na ni fursa yake ya kujitangaza.

‎Mwang’onda alisema mashindano hayo yalikuwa na ushindani mkubwa kutokana na kuwepo kwa wanawake ambao wana ujuzi wa muda mrefu wa kupika chapati.

‎”Ninajiendeleza katika fani ya mapishi Veta Chang’ombe, lengo langu niweze kujiamini wakati wa kupika, kutengeneza vitu vizuri na kuwa bora zaidi kwa mapishi mbalimbali ambayo yatanisaidia katika kuimarisha biashara na kuongeza kipato,” alisema.

‎Kwa upande wake, mwalimu wa mapishi kutoka Veta Chang’ombe, Euphrasia Mushi alisema ni vema mamalishe kujiendeleza katika fani hiyo ili kupata vyeti ambavyo vitawasaidia kutambulika, kujitangaza na kupata fursa ambazo zitajitokeza nchini.

‎Kwa upande wa mratibu wa mashindano hayo kutoka EATV, Anna Sombida alisema mashindano hayo yanalenga ‎kumwongezea mama lishe thamani na ‎uwezo katika kutimiza majukumu yake ‎ya kila siku.