Mwelekeo wa bajeti kwa mazao asilia ya biashara
“KATIKA mwaka 2025/2026 Wizara ya Kilimo itawawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao asilia ya biashara ya pamba, kahawa, mkonge, korosho, tumbaku, pareto, sukari, kakao na chai kutoka tani milioni 1.45 mwaka 2024. hadi tani milioni 2.22 mwaka 2025.”
“Uzalishaji wa pamba utaongezeka kutoka tani 149,361 hadi 400,000, kahawa kutoka tani 81,366 hadi tani 85,000, korosho kutoka tani 528, 263 hadi tani 700,000 na tumbaku kutoka tani 160,000 hadi tani 200,000.”
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe analiambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo katika Mwaka wa Fedha wa 2025/2026, Mei 21, mwaka huu.
Bashe anazungumzia baadhi ya mazao hao na mazao ya mafuta ya kula akianzia zao la pamba analosema mkakati uliopo katika wizara hiyo ni kujenga kongani ya pamba katika Mkoa wa Simiyu kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 1,000.

Anasema Wizara ya Kilimo ina mkakati wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata na kutengeneza pamba za hospitali na nyuzi kwa ajili ya kufungia tumbaku katika Mkoa wa Simiyu.
Kwa nini? Bashe anasema, “Hatua hiyo itaipunguzia nchi gharama ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 19.5 za kuagiza pamba za hospitali na nyuzi kwa ajili ya zao la tumbaku.”
Kuhusu zao la tumbaku, waziri huyo analiambia Bunge kuwa mkakati wa wizara ni kuainisha kiwanda cha kuchakata tumbaku tani 28 kwa siku katika Mkoa wa Tabora na kuanzisha bandari kavu kwa ajili ya kupaki tumbaku na anadokeza kuwa, mwekezaji ni Kampuni ya Mkwawa Leaf.
“Mkakati mwingine ni kuanzisha bandari kavu kwa ajili ya kuhifadhi na kufungasha tumbaku katika mikoa ya Morogoro na Tabora,” anasema Bashe na kuongeza: “Pia, kujenga mabani 2,500 kwa ajili ya kukaushia tumbaku na kuanza kutumia teknolojia ya jua na umeme katika ukaushaji wa tumbaku.”
Hotuba hiyo ya bajeti ya Wizara ya Kilimo inasema mkakati mwingine katika zao hilo ni: “Kununua mitambo minne ya kuchimba mabwawa na visima katika mashamba ya wakulima wadogo wa tumbaku katika mikoa ya Shinyanga na Tabora ili kuimarisha kilimo cha umwagiliaji.”
Kuhusu zao la parachichi, Bashe analiambia Bunge: “Wizara katika mwaka 2025/2026 itawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa parachichi kutoka tani 195,162 mwaka 2024/2025 hadi tani 250,000… Aidha, itaongeza mauzo ya parachichi nje ya nchi kutoka tani 35,627.02 zenye thamani ya Shilingi bilioni 252.3 hadi tani 50,000.”
Anasema malengo hayo yatafikiwa kwa kutekeleza mikakati kadhaa ukiwamo wa kuzalisha miche 2,100,000 kwa mpango wa ruzuku na kuweka mfumo wa usimamizi, uandaaji, usambazaji na utunzaji wa miche hiyo na kusaidia wakulima wadogo kupata miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya wakulima wadogo wa parachichi.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo ya bajeti iliyosomwa bungeni Mei 21, 2025, wizara pia ina mkakati wa kujenga vituo vitatu vya kufungasha parachichi katika mikoa ya Njombe na Mbeya.
Mkakati mwingine kwa mujibu wa hotuba hiyo ya bajeti ni: “Kujenga vituo 100 vya kukusanyia parachichi katika mikoa ya Njombe, Mbeya, Kilimanjaro na Iringa ili kuondoa madalali na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno pamoja na kutunga kanuni za kusimamia mnyororo wa thamani wa zao la parachichi kwa kutambua wanunuzi, mawakala, kusimamia bei elekezi na kuweka madaraja ya matunda.”

Bashe anasema: “Katika kuimarisha uongezaji wa thamani wa parachichi zinazozalishwa na wakulima wadogo na kuhakikisha hakuna daraja la parachichi litakalotupwa, wizara itaviwezesha viwanda vya uchakataji na utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na parachichi yakiwamo mafuta ya parachichi kwa ajili ya kusafirisha kwenda nje ya nchi.”
Kuhusu mazao ya mafuta, Bashe anasema uzalishaji wa mafuta ya kula umefikia tani 396,335 ikilinganishwa na mahitaji ya takribani tani 650,000 kwa mwaka.
“Uzalishaji huo unafanya taifa kuwa na nakisi ya tani 253,665 za mafuta ya kula,” anasema na kuongeza kuwa, ili taifa lijitosheleze kwa uzalishaji wa mafuta ya kula, wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora za alizeti tani 2,150 na kuzisambaza kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku.
Mengine ni kuzalisha na kusambaza kwa wakulima miche ya michikichi milioni 10 kwa wakulima kupitia mpango wa ruzuku. Mambo mengine serikali inasema kupitia Wizara ya Kilimo imepanga kuwezesha uchakataji wa mafuta
yatokanayo na alizeti na chikichi kwa kuwezesha viwanda vidogo vya wakulima.
Bashe anasema katika hotuba yake: “Wizara itaendelea kujadiliana na Wizara ya Fedha ili kuweka utaratibu wa kikodi kwa lengo la kuongeza kodi kwa mafuta yote yanayotoka nje ya nchi na kutengeneza utaratibu wa usimamizi wa kiutawala ili kulinda viwanda vya ndani na pia, itaanza majadiliano na Wizara ya Nishati kuweka ruzuku ya umeme kwenye kongani za viwanda vya mafuta ya kula katika mikoa ya Singida na Kigoma.”
Anasema msimamo wa wizara hiyo ni kuendelea kujadiliana na Wizara ya Fedha kuhusu kufanya mabadiliko ya sera za kodi ukiwamo uongezaji wa tozo katika mafuta ya kula na ngano zinazotoka nje ya nchi ili kulinda wakulima na viwanda vya ndani.”
Wadau mbalimbali wanasema hotuba hiyo inaleta tumaini jipya kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato kama bajeti hiyo itatekelezwa kama ilivyopangwa huku ikiongeza fedha za kigeni na kutoa ajira kwa Watanzania ama ya moja kwa moja, au zisizo za moja kwa moja katika kilimo.



