Mwenge wapongeza falsafa ya Rais Samia

KIGOMA: KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Ismail Ussi amesema kuwa miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali imeleta mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo kwa wananchi ikitekeleza falsa na maono ya Rais katika kuleta hali bora ya maisha kwa wananchi.
Ussi amesema hayo leo Septemba 16, 2025 akiwa wilayani Kibondo mkoani Kigoma siku ya pili ya ziara ya siku nane mkoani hapa.
Alibainisha kuwa Rais Samia ana mapenzi makubwa na wananchi wake ndiyo maana anapambana kuhakikisha wanapata maendeleo.

Ukiwa wilayani Kibondo, Mwenge wa Uhuru ulizindua madarasa manne na matundu sita ya vyoo katika shule mpya ya msingi Kilemba, uwekaji wa Jiwe la Msingi la barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa mita 470, kuweka jiwe la msingi la vibanda 66 vya biashara kwenye soko la samaki Kibondo mjini sambamba na ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Maloregwa.
Awali Mkuu wa wilaya ya Kibondo, Kanali Mstaafu Agrey Magwaza akipokea kwenye wa uhuru kutoka wilaya ya Kakonko alisema kuwa ukiwa wilayani humo mwenge huo wa uhuru utatembelea miradi saba yenye thamani ya shilingi Bilioni 3.1 ambapo serikali kuu imetoa kiasi cha Sh bilioni 2.1 na nguvu za wananchi Sh milioni 16.

Akiwa kwenye mradi wa ujenzi wa vibanda kwenye soko la samaki Kibondo Mjini Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa katika mradi huo jumla ya vibanda 66 vinajengwa sambamba na meza ambapo wafanyabiashara Zaidi ya 200 wanatarajia kunufaika na uboreshaji wa soko hilo.



