Mwigulu amsifu Samia kutimiza maono ya Nyerere

WAZIRI wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi aliyetimiza maono ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere ya kuifanya Tanzania kuwa taifa linalojitegemea kwenye uchumi.

Akizungumza jana Dar es Salaam kwenye mkutano wa kampeni za mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia, Dk Mwigulu amesema katika miaka mitano Samia ameshughulika na matatizo sugu yaliyokuwa yanawakabili Watanzania kwa kuhakikisha haki zao hazipotei.

Ameeleza kuwa, kwa mara ya kwanza Serikali ya Awamu ya Sita imeendesha uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu kwa fedha za ndani, hivyo ametimiza maono ya Nyerere ya Tanzania kuwa taifa linalojitegema. “Samia ni kiongozi anayejali utu na maslahi ya wananchi. Alipoingia madarakani, alielekeza wananchi waliokuwa wanadai fidia walipwe zaidi ya Sh bilioni 500.

Rais Samia amelipa madeni ya watumishi wa umma, amewapandishia mishahara na madaraja na ametoa ajira mpya bila kukwamisha shughuli nyingine za maendeleo, ikiwepo ujenzi na uendelezaji wa miradi mikubwa,” alisema Dk Mwigulu. SOMA: Nchimbi: Asiyempigia kura Samia hana nia njema

Amesema kazi zilizofanywa na Samia zinaonekana kwa vitendo na zinamnufaisha kila mwananchi, ikiwemo ununuzi wa madawati, ujenzi wa shule za msingi zaidi ya 2,700, sekondari zaidi ya 1,300, zahanati 2,800, vituo vya afya zaidi ya 600 na hospitali mpya zaidi ya 119.

“Dar es Salaam ni jiji la biashara, kuna wakati gharama zilikuwa kubwa sana kwa sababu ya kukosekana kwa umeme na mgao wa umeme lakini ulikamilisha haraka Bwawa la Mwalimu Nyerere lililogharimu Shilingi Trilioni 6.5 kwa fedha za ndani na kukamilika kwake kumeipeleka nchi kuwa na umeme wa ziada zaidi ya megawati 2,000,” alisema.

Dk Mwigulu amesema Samia alijenga mradi wa kuimarisha gridi ya taifa ambao umesababisha Watanzania wasahau mgao wa umemewa mara kwa mara, amenunua transfoma kubwa, ameongeza uwezo gridi ya kutoka Ubungo kwenda Chalinze, Gongo la Mboto, Mbagala na Makumbusho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button