Mwili wa mwanaume waokotwa B’moyo na majeraha shingoni

PWANI; MWILI wa mtu ambaye jina lake halifahamika mwenye miaka kati ya 40 hadi 50 umeokotwa huku ukiwa na majeraha ya kitu chenye ncha kali shingoni.
Hayo yalisemwa na Mjini Kibaha na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase. Alisema waliupata mwili huo Januari 4 mwaka huu alfajiri katika Kijiji cha Zinga, Kata ya Zinga wilayani Bagamoyo.
Morcase alisema mwili huo ulikutwa na watu wanaoamka alfajiri wakati wakielekea kuokota maembe Kijiji cha Zinga kisha kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji ambaye naye alitoa taarifa Polisi.
“Watu hao walikuwa wameenda kuokota maembe waliona mwili wa mwanaume huyo akiwa amevaa kaptura bila ya nguo nyingine mwilini, siyo jambo la kawaida mtu kufanyiwa tukio hilo, inaonekana hapo kuna jambo nyuma yake,” alisema Morcase.
Alisema taarifa iliwafikia Polisi Wilaya ya Bagamoyo na walipofika wakiwa na wataalamu walibaini kuwa mwili huo ulikuwa na majeraha hayo.
“Polisi walibaini kuwa na mburuziko hali ambayo inaonekana mtu huyo aliletwa na kutupwa hapo ambapo kuna kichaka,” alisema Morcase.
Aidha, alisema kama kuna mtu anandugu yake aliyepotea afike kituo cha Polisi Bagamoyo au kituo chochote cha Polisi na wananchi watoe taarifa pale wanapotilia shaka wanapoona matukio kama hayo na wao ni wataalamu watachambua.



