Mwinyi afunga kampeni Pemba, aeleza vipaumbele 10 vya maendeleo

MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, amehitimisha kampeni zake Kisiwani Pemba, kwa kueleza vipaumbele 10 vitakavyoongoza safari ya maendeleo ya Zanzibar katika miaka mitano ijayo endapo atapewa ridhaa ya kuiongoza kwa muhula wa pili.

Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni hiyo, Dk. Mwinyi amesema vipaumbele hivyo vinalenga kuendeleza umoja wa Wazanzibari, kukuza uchumi jumuishi, na kuboresha maisha ya wananchi wote wa visiwani humo.

Dk. Mwinyi amesema Serikali itajikita katika kuimarisha umoja, amani, na maridhiano miongoni mwa Wazanzibari ili kudumisha utulivu na mshikamano. “Zanzibar imetoka mbali, tunapaswa kuendelea kulinda amani, kuvumiliana na kushirikiana ili tufikie malengo ya maendeleo tuliyoyapanga,” alisema.

Miongoni mwa vipaumbele alivyoainisha ni kuimarisha uchumi unaonufaisha makundi yote, na kuongeza fursa za ajira kwa vijana. Amesema Serikali inalenga kuzalisha ajira 350,000 katika sekta rasmi na zisizo rasmi ifikapo mwaka 2030. “Kila kijana atapatiwa nafasi ya kutumia uwezo wake. Tutahakikisha kila sekta inachangia katika kuunda ajira mpya,” alisisitiza.

Vipaumbele vingine ni kuhakikisha uhakika wa chakula kupitia hifadhi ya taifa ya chakula, pamoja na kuongeza uzalishaji wa ndani.Dk. Mwinyi pia ameahidi kuimarisha uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kupitia mikopo, mafunzo ya umahiri na matumizi ya teknolojia katika biashara na uzalishaji.

Katika kipindi kijacho, Serikali inalenga kuanzisha makaazi bora na miji ya kisasa, ikizingatia teknolojia mpya ya ujenzi, mipango miji, na usafi wa mazingira, ili kuboresha maisha ya wananchi wa Zanzibar mijini na vijijini. Dk. Mwinyi ameahidi kuanzisha hifadhi ya kitaifa ya mafuta ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa bidhaa hiyo na kupunguza athari za mabadiliko ya bei duniani.

Pia, ameweka mkakati wa kuweka vivutio maalumu vya uwekezaji katika sekta kuu za uchumi kama uchumi wa buluu, viwanda, kilimo na huduma. Rais Mwinyi alisema Serikali yake itaendelea kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu, maji safi, umeme na afya.

Kipaumbele kingine ni kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wote, hasa wazee na watu wenye mahitaji maalum. Kwa ujumla, kupitia vipaumbele hivyo 10, Dk. Mwinyi ameonesha dhamira ya kujenga Zanzibar yenye uchumi imara, usawa wa fursa na ustawi wa wananchi wote bila kumwacha mtu nyuma. “Ninaamini katika Zanzibar yenye umoja, maendeleo na fursa kwa wote. Hiyo ndiyo dira yangu kwa miaka mitano ijayo,” alisema Mwinyi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button