Mwinyi awaomba kura wauza samaki,wajasiriamali

ZANZIBAR : MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameendelea na kampeni zake kwa kutembelea soko kuu la Malindi, Mji Mkongwe, ambapo alizungumza na wajasiriamali na wauza samaki.
Katika ziara hiyo ya asubuhi ya Jumanne, Septemba 30, 2025, Dk. Mwinyi alieleza kufurahishwa na mapokezi ya wananchi na kuahidi kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuendeleza sekta za uvuvi na ujasiriamali.
“Nimefurahi sana kukutana nanyi. Naomba kura zenu kwangu, kwa mama Samia Suluhu Hassan na wagombea wengine wa CCM. Niliyoyaahidi mwaka 2020 nimefanikiwa kuyatekeleza, na sasa naomba tena miaka mitano ijayo ili tuzidi kushirikiana katika kuleta neema zaidi,” alisema Dk. Mwinyi.
Alifafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali yake imetoa mikopo isiyo na riba, maboti kwa wavuvi pamoja na vifaa vya kilimo cha mwani, hatua ambayo ni mwanzo wa safari ndefu ya kuwawezesha wavuvi na wakulima kuongeza kipato.
Aidha, alibainisha kuwa serikali inaendelea kujenga masoko na madiko mbalimbali Unguja na Pemba ili kutoa maeneo bora ya kufanyia biashara. SOMA: Dk. Mwinyi asema ahadi za serikali zinatekelezwa
“Tumeahidi mazingira mazuri ya biashara na tutaendelea kuyajenga. Tutawasaidia wavuvi kufika bahari kuu kuvua kwa wingi, na wajasiriamali nao watapata nafasi ya kuendesha shughuli zao katika mazingira safi na yenye usimamizi bora,” aliongeza.
Dk. Mwinyi pia alikumbusha kuwa serikali imetenga shilingi bilioni 96 kwa ajili ya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ingawa baadhi yao bado hawajafikiwa. Alisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha kila mmoja ananufaika na mipango hiyo.
“Hakuna sababu ya kukosa usafi na usimamizi katika masoko yetu. Tukipata fedha zaidi tutajenga masoko ya kisasa na kuimarisha mazingira bora ya biashara,” alisema huku akitoa agizo kwa Shirika la Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) kuhakikisha masoko yote ya samaki yanakuwa safi.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wa Malindi wakiongozwa na Nia Juma Mbwana walipokea kwa matumaini makubwa ahadi hizo, wakisema sekta ya uvuvi na biashara ya samaki inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar na kuboresha maisha ya wananchi wake.