Mwinyi: Pigeni kura Oktoba 29

UNGUJA : MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi kupuuza kauli za wanasiasa wanaoshawishi kujitokeza kupiga kura Oktoba 28, akibainisha kuwa siku hiyo ni maalum kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni Bubwini, Dk. Mwinyi alisema siku ya kupiga kura kwa wananchi wote ni Oktoba 29 na kuongeza kuwa kushawishi wananchi kujitokeza Oktoba 28 ni kuchochea fujo. Alisema sheria ya uchaguzi imeainisha kuwa vyombo vya ulinzi hupiga kura mapema ili siku ya uchaguzi wawe huru kulinda amani.

“Mtu akikwambia utoke kupiga kura Oktoba 28 usikubali, hiyo siku ni kwa watu waliotajwa kisheria, nyinyi jitokezeni Oktoba 29,” alisema. Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa ajenda ya CCM ni kudumisha amani, mshikamano na maridhiano, akiwataka wananchi kuendeleza misingi hiyo kabla na baada ya uchaguzi.

Akizungumzia miradi ya maendeleo, alisema serikali itaendelea kuimarisha sekta ya elimu na maji, ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya, skuli, na matangi makubwa ya kuhifadhi maji. Aidha, alitaja ujenzi wa Bandari ya Mangapwani kuwa ni mradi mkubwa wa kimkakati utakaochangia kukuza uchumi wa Zanzibar.

Alibainisha kuwa serikali imetenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia wananchi waliopisha ujenzi huo na kwamba watakaotaka nyumba mpya badala ya fedha watapatiwa makazi bora. “Mkituchagua tena tutakamilisha miradi hii na kuwaletea maendeleo zaidi,” alisema.

Katika mkutano huo, wanachama 28 wa ACT Wazalendo walihamia CCM, huku Naibu Katibu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohammed Said Mohammed, akiwaomba wananchi kumpa ridhaa Dk. Mwinyi kwa muhula mwingine wa uongozi. SOMA: Samia: Tuna akiba ya kutosha ya chakula

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button