Mwongozo uwezeshaji wanawake wazinduliwa

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dk Dorothy Gwajima leo amezindua rasmi mwongozo wa uundaji na uratibu wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi ikiwa na lengo la kuwafikia wanawake wote hadi maeneno ya vijijini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Dk Gwajima pia amezindua rasmi kamati ya kuratibu suala la kuelimisha na kuhamasisha wanawake kujiunga na jukwaa hilo hafla ambayo imeandaliwa Benki ya Biashara ya Tanzania(TCB).
“Hapa wanaratibu Masuala ya elimu na uwezeshaji wanawake kiuchumi na yanalenga majukwaa ambayo Rais samia alianzisha,tunahesabu kila kijiji kuna vikundi vingapi ili tuweze kuwaunganisha na wadau kufanya kazi pamoja.
Dk Gwajima amesema kamati hiyo inafanya kazi na wadau mbalimbali wa sekta zote zenye jukumu la kujenga fursa kwa wanawake ikiwemo TCB benki na zingine.
“Kuna wanawake wengi wanajishughulisha na biashara na ujasiriamali hivyo wadau wote wataingia katika hili na tunawashukuru TCB benki kwa hili lakini na pia tunawaalika wadau wengine wawawezeshe wanawake,”amesisitiza.
Aidha amesema katika uwezishaji wanawake pia wanaangalia visababishi vya wanawake kurudi nyuma na wanawapa semina ya afya ya akili ,migogoro na ukatili wa kijinsia hivyo na wanaume wanaingia kwenye mikakati ya kisera.
Amesema licha ya kupata semina za uchumi pia wanajifunza namna bora ya malezi na makuzi kwa watoto hivyo wanataka washeheni maarifa na sio uchumi tu.
Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Biashara ya TCB Adam Mihayo amesema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya fedha hivyo Benki itaendelea kuunga mkono miradi ya kimkakati inayotekelezwa na serikali katika kuinua uchumi wanawake na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake rais wa Mabenki,Tusekelege Mwaikasu amesema mwongozo huo utaleta majibu na kusaidia mabenki namna ya kutekeleza maendeleo wa miaka 10 ya sekta ya fedha.
“Niendelee kusisitiza kama sekta benki hili ni letu na tutaendelea kuwa pamoja hivyo niahidi kuwa tutakuwa wote kila wakati.



