MWONGOZO WA MALEZI: Msingi wa urithi wa familia bora
MALEZI ya Watoto katika familia ni suala linalohitaji kupewa kipaumbele na wazazi, walezi, familia, jamii na taifa kwa ujumla kwa sababu watoto ni taifa la baadaye.
Watoto pia wanahitaji kuandaliwa vya kutosha katika makuzi na maendeleo yao kwa ajili ya ustawi wa maisha yao.
Kwa miaka iliyopita, malezi ya watoto yalikuwa yakifanyika kwa ushirikiano baina ya wazazi wa mtoto na wanajamii wengine kwa ujumla. Ushirikiano huo ulisaidia kulinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili, vitendo na mambo yasiyofaa pamoja na athari nyingine zinazohatarisha ustawi na maendeleo yao.
Vyanzo mbalimbali vinathibitisha kuwa, kumomonyoka kwa mfumo huo wa malezi kumesababisha watoto wengi kuwa katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili na kujiingiza katika makundi ya watoto walio katika mazingira hatarishi.
Ni kutokana na umuhimu huo na katika kuimarisha malezi ya watoto na familia nchini, hivi karibuni serikali imezindua ‘Mwongozo wa Taifa wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Vikundi vya Wazazi vya Malezi na Matunzo ya Mtoto.’
Aidha, serikali ilizindua kitini cha Elimu ya Malezi ya Familia kwa Ajili ya Kuzuia Vitendo vya Ukatili Dhidi ya Watoto Tanzania (2015) kilichotumika kuwajengea uwezo watalaamu wa ngazi za mikoa na halmashauri waliotoa elimu ya malezi chanya kwa wazazi na walezi kwa mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Akizungumza baada ya kuzindua mwongozo huo na kufunga Kongamano la Malezi katika Siku ya Kimataifa ya Familia, lililoadhimishwa kitaifa katika manispaa ya Ilemela, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko anaitaka jamii kufahamu kuwa, familia ni chanzo cha maendeleo ya jamii duniani.
Anasema ni lazima kuitambua na kuienzi taasisi hiyo muhimu ya familia kutokana na majukumu mengi iliyonayo. Dk Biteko aliyemwakilisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango anasema jamii inatakiwa kutoa huduma muhimu ili kukidhi mahitaji ya watoto na familia sambamba na kusimamia malezi na makuzi mema ya watoto.
Anasema familia ina jukumu la kurithisha mila na utamaduni mzuri kwa watoto na familia kwa ujumla kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine. Anasema sherehe za maadhimisho ya Siku ya Familia kwa mwaka huu zimefanyika katika ngazi ya mikoa, wilaya, kata, vijiji na mitaa zikiongozwa na kaulimbiu: ‘Mtoto ni Malezi; Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara.’
Anasema ili kuimarisha malezi bora kwa watoto chini ya miaka minane, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa na inatekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa kipindi cha 2021/22 – 2025/26.
Anasema programu hiyo inahakikisha watoto wanapata huduma stahiki na jumuishi za malezi kwa uwiano sawa tangu mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake hadi anapofikisha umri wa miaka minane.
Anasema ili kuimarisha uelewa wa programu hiyo muhimu kwa jamii na katika kipindi husika, serikali imeratibu na kusimamia mafunzo kwa maofisa zaidi ya 6,000 wa sekta za afya, elimu, lishe, ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii na watoa huduma wengine ngazi ya jamii kwenye mikoa yote 26 na halmashauri 184.
Anasema katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa programu hiyo, serikali imewajengea uwezo walimu wa awali 12,000 kutoka halmashauri 184 kutoa elimu ya malezi chanya ya watoto, wakihudumia zaidi ya watoto 360,000.
Anasema serikali imejenga vituo vya kulelea watoto wadogo mchana 4,178, kutoa huduma za malezi na elimu ya awali kwa zaidi ya watoto 400,000 sanjari na kuanzisha vituo vya kijamii 206 vinavyomilikiwa na jamii yenyewe vimeanzishwa vikitoa huduma kwa watoto 11,675.
Naibu Waziri Mkuu anasema watoto wanapolelewa katika malezi na makuzi bora, huwa na uwezo wa kutengeneza familia bora yenye uwezo wa kufanya kazi, kushiriki shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Anazungumzia umuhimu wa jamii kuondokana na migogoro ya kifamilia kwa kuwa haina tija kwa ustawi wa familia na hata kwa watoto wenyewe kwa madai kuwa, hawana sababu ya kuingizwa kwenye migogoro hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Abeida Rashid anasema malezi ya awali ya mtoto ni msingi wa malezi bora kwa makuzi ya watoto.
Anasisitiza kuwa, SMZ imepiga hatua kubwa kuhakikisha watoto wanakua katika makuzi na malezi bora. Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ally Khamisi anasema maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia mwaka huu yanasisitiza umuhimu wa malezi bora kwa watoto ikiwa ni msingi wa familia bora inayolenga kuwa na taifa imara.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Taifa wa Malezi na Makuzi (TECDEN), Elizabeth Thobias anasema suala la malezi bora kwa watoto katika jamii ni msingi imara katika kuendeleza taifa. “Kwa kutambua umuhimu huo,” anasema mwaka 2021 serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilizindua Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM).
Anasema lengo la programu hiyo lilikuwa kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anakuwa katika mwelekeo sahihi wa ukuaji ili kufikia ukuaji timilifu. Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu, Biteko, Ripoti ya Utafiti wa Afya na Watu na Viashiria vya Maleria (TDHSMIS, 2022) ni asilimia 47 pekee ya watoto wa Kitanzania walio kwenye mwelekeo sahihi wa ukuaji wao.
“Hii inatupa ishara kuwa ipo kazi kubwa kuhakikisha asilimia 53 ya watoto ambao hawako kwenye mwelekeo sahihi wa ukuaji wao, nao wanafikiwa,” anasema.
Anasema katika utekelezaji wa programu hiyo, TECDEN inaendelea kuchagiza uratibu wa wadau wasio wa kiserikali katika ngazi ya kitaifa, mikoa pamoja na halmashauri kupitia mashirika wanachama wake ambao mpaka sasa wapo takribani wanachama 122.
Hayo ni pamoja na mashirika yasiyo ya serikali yanayotekeleza shughuli zake nchini, mashirika ya kimataifa na wadau mbalimbali wa maendeleo. Mtandao huo una mashirika waratibu wa programu ya MMMAM katika mikoa yote 26 Tanzania Bara.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) –Tanzania, Laxmi Bhawani anasema maendeleo ya awali ya watoto si suala la malezi tu, bali ni pia mabadiliko ya kitaifa. Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, suala hilo ndilo linalounda mwelekeo wa maisha ya watoto, kuathiri ustawi wao, uwezo wao wa kujifunza na mchango wao wa baadaye katika jamii.
Anasema Unicef inapongeza Serikali ya Tanzania kwa kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya awali ya watoto kupitia mpango wa kitaifa wa sekta mbalimbali wa ECD na mpango wa usawa wa kijinsia.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk John Jingu anasema elimu ya malezi ya watoto iliwapa hamasa wazazi na kuamua kuanzisha vikundi vya wazazi vya malezi katika baadhi ya vijiji na mitaa nchini.
Kwa mujibu wa Dk Jingu, miaka minne iliyopita wizara hiyo ilifanya tathimini ya programu ya malezi sambamba na ufanisi wa vikundi vya wazazi vya malezi vilivyoanzishwa ili kuona utekelezaji wa programu hiyo.
Anasema tathmini hiyo ilibainisha uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo uchache wa vikundi vya malezi katika jamii, ushiriki mdogo wa wanaume na kukosekana kwa uwiano katika uanzishwaji na uendeshaji wa vikundi.
Changamoto nyingine ni wananchi kukosa hamasa ya kujiunga kwa sababu ya kutolewa kwa elimu ya malezi pekee jambo linalokosa uzito wa kumshawishi mzazi au mlezi kujiunga na kikundi husika.
Maeneo muhimu
Mwongozo huo umeainisha maeneo kadhaa muhimu. Sura ya kwanza inaelezea utangulizi kuhusu shughuli
mbalimbali ambazo zimekuwa zikitekelezwa na serikali hususani katika programu mbalimbali za utoaji elimu ya
malezi ya watoto na familia katika jamii.
Aidha, sura hiyo inaeleza jitihada za serikali kuimarisha malezi, ulinzi na usalama wa mtoto. Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanya jitihada mbalimbali za ulinzi na usalama wa mtoto ikiwa ni pamoja na kuridhia na kusaini mikataba ya kikanda na kimataifa, kuandaa sera na miongozo na kutunga sheria.
Sura ya pili inaelezea uanzishaji na uendeshaji wa kikundi cha wazazi cha malezi. Kwamba, kiwe kilianzishwa kwa makubaliano ya hiari ya wazazi au walezi kupatia hamasa na elimu ya malezi chanya na kukubali kushirikiana katika shughuli za malezi, makuzi na maendeleo ya watoto katika jamii.



