Mzumbe yashauriwa kujipanga kimataifa elimu ya juu

CHUO Kikuu Mzumbe (MU) kilichopo mkoani Morogoro kimeshauriwa kuimarisha uhusiano na mashirikiano kimataifa ili kiweze kupata wanafunzi kutoka nje ya nchi na kutoa wahadhiri wataoenda kufundisha vyuo vya nje.

Katibu mkuu kiongozi mstaafu, Philemon Luhanjo ametoa ushauri huo alipokuwa mgeni rasmi katika Baraza la 25 la wahitimu wa Chuo Kikuu hicho.

Luhanjo amesema kwa ukongwe wa Chuo hicho katika kutoa elimu ya juu nchini ni muhimu sasa kuongeza nguvu kimataifa.

“Ninaisihi menejimenti ya chuo kuongeza mashirikiano na mashirika ya nje ya nchi, tunataka kuona sifa zinazotolewa juu ya umahiri wa chuo hiki zinatuletea wanafunzi wengi kutoka mataifa ya nje” amesema Luhanjo.

Licha ya hayo ameishauri menejimenti hiyo kuongeza ushawishi kwa wahitimu wa wake kujiunga katika Baraza hilo ili kuongeza nguvu kwenye kufanikisha mipango mbalimbali ikiwemo kusaidia ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanatoka katika mazingira magumu.

“Nimevutiwa na huu mpango wa Baraza la wahitimu kufadhili masomo kwa wanafunzi wasio na uwezo wa kumudu gharama za chuo.”

“Katika kuunga mkono mpango huu mimi binafsi ninachangia Sh milioni kumi, tunapaswa kuongeza nguvu katika hili ili kupata wahitimu wengi ambapo wanapitia kusoma chuo Kikuu Mzumbe” amesema Luhanjo.

Luhanjo amewashauri wanafunzi kuwa na imani na chuo hicho kwani kimeendelea kuzalisha viongozi wa ngazi za juu nchini.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa MU, Profesa William Mwegoha amesema chuo kimejipanga kuongeza ushirikiano wa kimataifa na kuboresha mitaala ambayo itatoa chachu kupokea wanafunzi kutoka nje ya nchi, ukiwa ni mkakati wa kukuza ubora wa elimu na kuongeza mapato.

Profesa Mwegoha amesema mpango huo unalenga kuongeza idadi ya wanafunzi wanaokwenda nje ya nchi na wale kutoka mataifa mengine kuja kusoma Chuo Kikuu Mzumbe, hatua itakayokifanya chuo kuwa na hadhi ya kimataifa na kuongeza ushindani katika soko la elimu ya juu.

Katika hatua nyingine Baraza la wahitimu la 25 limepitisha katiba yake na hivyo litaweza kuendesha shughuli zake pia itasaidia kusimamia miradi mbalimbali ikiwemo kusaidia ufadhili wa masomo kwa wanafunzi.

“Kwa mwaka huu tumeanza na wanafunzi wawili kuwafadhili na kadri tunavyoendelea tutaongeza idadi ya wanafunzi, ” amesema Profesa Mwegoha.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button