Nacopha yaridhishwa na juhudi za serikali udhibiti VVU

BARAZA la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA) limeeleza kuridhishwa na hatua za serikali ya awamu ya sita kudhibiti maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) mbali na mabadiliko ya sera za wahisani.

Mwenyekiti wa NACOPHA Tanzania, Leticia Kapela alitoa kauli hiyo Julai 25, 2025 mjini Geita katika mkutano maalum na waandishi wa habari na kukiri wazi kuwa huduma zinazoedelea kutolewa zinatia matumaini.

Kauli yake inakuja ikiwa ni miezi sita tangu Rais wa Marekani, Donald Trump alipotangaza kupunguza ufadhili wa Shirika la Msaada la Marekani (USAID) ikiwemo kufadhili ARVs kupitia mpango wa PEPFAR.

Leticia amekiri mbali na sera za USAID kubadilika bado serikali imehakikisha watanzania wanaendelea kupata huduma za VVU na UKIMWI ikiwa ni pamoja na tiba, vitendanishi na huduma kinga.

Amesema NACOPHA imefurahishwa na jinsi serikali ilivyohakikisha uwepo wa bajeti ya kutosha kwa huduma za afya na VVU nchini ikiwemo kujenga uwezo wa ndani kupitia mfuko wa Mwitikio wa ukimwi.

Ameongeza, pia mpaka sasa serikali imefanikiwa kuimarisha mahusiano na sekta binafsi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uwepo wa mikakati ya kufufua viwanda vya kutengeneza dawa za ARVs.

Amesema NACOPHA inatambua kuwa serikali ya awamu ya sita imeweka malengo ya kimkakati ya kuimarisha uwezo wake wa ndani kujitosheleza kununua dawa za kutosha kila mwaka kwa watu walio kwenye tiba ya VVU.

“Hii imeondoa wasiwasi na mashaka kwa walio kwenye tiba ya ARVs kutokupata tiba hiyo baada ya wafadhili kujiondoa au kupunguza ufadhili wao”, amesema Leticia.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Deogratius Rutatwa amewataka watanzania kuachana na habari zinazowatia hofu watu wanaoishi na VVU baada ya sera za USAID kubadilika kwani serikali ipo imara.

Amedokeza kuwa, mpaka sasa NACOPHA imearifiwa Tanzania inaendelea kufuatilia upatikanaji wa dawa mpya ya VVU(sindano) iliyogunduliwa hivi karibuni na kuthibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Rutatwa amesema kutokana na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali hakuna haja ya kuwa na hofu kwenda kupima na kuhudhuria kliniki ya VVU kwani ipo mipango madhubuti kuimarisha huduma stahiki.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button