WANANCHI wa Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara wamejitokeza kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi mbalimbali wa serikali za mitaa wataowaletea maendeleo katika maeneo yao.
Akizungumza baada ya kupiga kura katika kituo cha kupigia kura cha mtaa wa Kilimanjaro kata ya Nanyamba, msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani humo, Mhandisi Mshamu Munde amesema zoezi la upigaji kura linaendelea vizuri na hakuna viashiria uvunjifu wa amani.
Uchaguzi huo wa serikali za mitaa umefanyika Novemba 27, 2024 kwa kuchagua viongozi katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo wenyeviti pamoja na wajumbe kupitia ngazi mbalimbali ikiwemo vijiji, vitongoji na mitaa.
Aidha vyama vinavyoshiriki zoezi hilo ni vinne kwenye halmashauri hiyo ikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, ACT Wazalendo pamoja na Chama cha Wananchi (CUF) ambapo hamasa ya kushiriki kugombea ilikuwa kubwa na wanarajia amani itaendelea kudumishwa.
Amesema:‘’Zoezi la kampeni lilienda vizuri kutokana na uwepo wa hali ya amani kwa kuwa hakukuwa na kesi hata moja ya maadili na idadi ya vituo vya kupigia kura ni 341 na jumla ya wapiga kura ni 65 elfu kwenye halmashuri hii ya Nanyamba,’’amesema Munde.
Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa mtaa wa Kilimanjaro kata ya Nanyamba kwa tiketi ya CUF, Abdilah Ally ‘’mpaka sasa zoezi hili linaenda vizuri kwani hakuna changamoto yoyote ile iliyojitokeza’’
Hata hivyo wakala na Mwenyekiti wa CUF kwenye halmashauri hiyo, Saidi Abdallah amesema wananchi wamehamasika na wamejitokeza kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya kupigia kura.
Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa serikali za mitaa katika mtaa wa Natoto kata ya Dinyecha kwa tiketi ya CCM, Fatuma Akili ametoa rai kwa wananchi wa mtaa huo na maeneo mengine wajitokeze kwa wingi wapige kura ili wawachague viongozi wanaowataka wataowaletea maendeleo katika maeneo yao.