Nape: Miaka 3 ya Samia kuna mabadiliko mawasiliano

DAR ES SALAAM: Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, amesema miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya mawasiliano ambayo iliundwa kwa mkakati maalum ili kuendana na kasi ya teknolojia na utandawazi.

Nape ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake na Balozi wa Finland nchini Theresa Zitting na kwamba awali sekta hiyo ilikuwa ndogo ndani ya dude kubwa, hivyo haikupewa kipaumbele inavyostahili.

“Miaka mitatu ya Rais Samia, kuna mabadiliko makubwa ya sera, kanuni, ujenzi wa kituo cha data, Mkongo wa Taifa na mpaka sasa kuna minara 771 sawa na asilimia 90 ya maeneo yote nchini kufikiwa na mtandao,”amesema Nape.

Amesema tayari wameweka sheria mpya ya watoa huduma wa simu za mkononi kutumia minara yote (Roming) ukiwa na laini ya simu A uweze kutumia moja kwa moja laini uliyonayo na kwamba hakuna haja ya kuwa na utitiri wa laini za simu.

Aidha, amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Finland katika kuimarisha hali ya mawasiliano hapa nchini ikiwemo ulinzi wa taarifa binafsi na usalama wa mtandao (Cyber Security ).

Amesema Finland ni moja ya mataifa yaliyopiga hatua kubwa katika maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) na kwamba huwezi kuzungumzia mafanikio ya Tanzania katika Tehema bila ya kuihusisha Finland ambayo imesaidia katika kutunga sera, sheria uwezeshaji wa watu, fedha na miundombinu.

Kwa Upande wake Balozi wa Finland nchini Tanzania Theresa Zitting amesema ushirkiano huu ni mwendelezo wa ushirikiano ulioanza miaka mingi iliyopita

Amesema nia ya Finland ni kuisaidia serikali ya Tanzania katika mitandao ikizingatiwa dunia kwa sasa ni kijiji na kwamba Tanzania ikiwa salama na nchi jirani zinazoizunguka zitakuwa salama na hata Finland itabaki salama

Habari Zifananazo

Back to top button