Ndugulile afariki dunia akiwa na miaka 55

Ndugulile alichaguliwa Agosti 27 mwaka huu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika, Nafasi aliyopaswa kuanza kuitumikia rasmi mwakani.

DODOMA – Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mkuu mteule wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile amefariki dunia akiwa na miaka 55.

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ametangaza kifo cha kiongozi huyo aliyekuwa India kwa matibabu kupitia Taarifa kwa Umma iliyochapishwa na Ofisi ya Bunge.

Ndugulile alichaguliwa Agosti 27 mwaka huu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika, Nafasi aliyopaswa kuanza kuitumikia rasmi mwakani.

Advertisement

Katika taarifa ya Dk Tulia ambayo haikutaja chanzo cha umauti wa kiongozi huyo, imesema, Ofisi ya Bunge itashirikiana na familia kuratibu zoezi zima la mazishi ya Ndugulile.

Rais Samia amlilia

Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge na familia ya Ndugulile akisema amepokea kwa masikitiko taarifa za msiba huo.

“Ninatoa salamu za pole kwa familia, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wa Kigamboni, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote,” ameandika Rais Samia.