Ngajilo aahidi kituo cha afya Uyole kuanza kazi ndani ya siku 100

IRINGA: MGOMBEA  ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya CCM, Fadhili Ngajilo, amepeleka ujumbe kwa Mkurugenzi na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Iringa kuhakikisha kituo cha afya cha Uyole kinaanza kutoa huduma ndani ya siku 100, akisisitiza haiwezekani fedha za serikali zitumike bila wananchi kunufaika.

“Tunapeleka ujumbe kwa mkurugenzi na mganga mkuu wa manispaa: nikichaguliwa ndani ya siku 100 tunataka kituo hicho kianze kufanya kazi. Haiwezekani fedha za serikali zitumike halafu kituo kisifanye kazi,” Ngajilo alisema huku akishangiliwa na mamia ya wakazi wa Kitwiru.

Katika mkutano wa kampeni uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM wakiwemo Mratibu wa Kampeni wa Jimbo hilo, Salvatory Ngerela, na Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa Said Rubeya, Ngajilo alibainisha kuwa maendeleo hayaji bila ushirikiano wa karibu kati ya viongozi na wananchi.

Aliahidi pia kufuatilia ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga daraja la Kitwiru-Isakalilo, litakalounganisha Kitwiru na sehemu nyingine za manispaa, pamoja na kushughulikia changamoto za maji, mawasiliano ya simu, barabara za mitaa na madampo.

Ngajilo aliwataka wananchi wa Iringa Mjini kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa Rais, wabunge na madiwani wa CCM, akisema kura nyingi ndizo zitakazoongeza hamasa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake mgombea udiwani wa Kata ya Kitwiru, Rahim Kapufi, alieleza namna atakavyoshughulikia changamoto mbalimbali za kata hiyo ikiwa ni pamoja na mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na walemavu, urasimishaji wa makazi, pamoja na kuboresha barabara za vumbi ili ziweze kupitika muda wote.

Rubeya na Ngerela waliwahimiza wananchi kutoacha haki yao ya kupiga kura, wakisisitiza kuwa “CCM ina njaa kali ya kuwaletea Watanzania maendeleo, na sasa baadhi wameanza kutuonea wivu.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button