Ngajilo aeleza mipango itakayofanikisha Iringa kuwa jiji

IRINGA: Fadhil Ngajilo, mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Iringa Mjini, ameweka wazi mkakati wa kuubadilisha mji wa Iringa na kuusogeza hatua kwa hatua kuwa jiji kamili, kwa kuimarisha huduma za kijamii, kuendeleza miundombinu na kuanzisha viwanda vya kimkakati.

Akihutubia mkutano wa kampeni katika kata ya Nduli, Ngajilo alisema mchakato wa kuifanya Iringa kuwa jiji ni “vita ya maendeleo” inayohitaji mipango madhubuti na mshikamano wa wananchi.

“Najua itachukua muda, lakini ni lazima tuingie kwenye vita ya kuigeuza manispaa kuwa jiji,” alisema.

Ngajilo alibainisha kuwa Nduli ni eneo la kimkakati kwa sababu lina Uwanja wa Ndege wa Iringa, ambao unaweza kutumika kusafirisha mazao ya kilimo kama parachichi kwenda masoko ya kitaifa na kimataifa.

“Nitahakikisha miradi ya kimkakati inatekelezwa na kuwanufaisha wananchi, kuwepo kwa uwanja wa ndege Nduli na kuanzisha kongani ya viwanda kutazalisha bidhaa ndogo ndogo, kuongeza ajira na kuchochea pato la manispaa,” alifafanua.
Ameongeza kuwa huduma za kijamii kama masoko na miundombinu ya barabara za lami zitasogezwa karibu na wananchi.

“Sio kazi ya Rais kupeleka maji au umeme kwa mwananchi mmoja mmoja. Hiyo ni kazi tutakayofanya sisi wabunge kwa kushirikiana na wananchi. Rais atapeleka mambo makubwa kama barabara za lami,” alisema.

Akizungumzia kilimo, Ngajilo aliahidi kupambana kuhakikisha mbolea bora inawafikia wakulima kwa wakati, akitambua changamoto za pembejeo zinazokabili wakulima wengi pembezoni mwa Iringa Mjini.

Katika mkutano huo, Meya Mstaafu Ibrahim Ngwada, alisisitiza umuhimu wa kushughulikia migogoro ya ardhi na kutoa wito kwa diwani kushirikiana na halmashauri kutatua changamoto hizo.

Pia alimuomba Ngajilo kufuatilia suala la fidia kwa shule ya msingi Nduli iliyosimamishwa kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege.

“Tunaomba utakapopata ubunge upambane tupate fidia ya kujenga shule nyingine yenye hadhi kubwa zaidi,” alisema.

Wananchi walimpongeza Ngajilo kwa kuwa kiongozi asiye na majivuno na mwenye kuunganisha jamii.

Leons Marto, aliye tia nia udiwani wa kata hiyo ya Nduli, aliwataka wakazi wa Nduli kupuuza upinzani usio na sera na kuunga mkono ajenda za maendeleo kupitia CCM.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button