Ngorongoro wajawa matumaini serikali ya CCM

ARUSHA: JAMII ya kifugaji ya kimasai wilayani Ngorongoro imeonyesha imani kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan, wakitarajia kwamba hatua za Serikali kupitia tume iliyoundwa kuchunguza masuala ya Hifadhi ya Ngorongoro na Pori Tengefu la Akiba la Pololeti zitaleta suluhisho la upatikanaji wa malisho ya mifugo kwa jamii hiyo.

Wakizungumza wakati wa ziara ya kampeni ya kuomba ridhaa kwa wagombea wa CCM katika kata za Oloipiri, Suitsambu na Olo olo sokwan, viongozi wa jamii kifugaji ya kimasai na wagombra hao wamesisitiza kuwa wana matumaini makubwa na majibu ya tume, na kwamba Oktoba 29 mwaka huu wako tayari kumpigia kura mgombea Urais wa CCM ,Rais Samia kwa kuwa wana  imani kuwa atatatua changamoto zao bila ya matatizo.

Diwani mteule wa kata ya Oloipiri, Latajewo Sayori, amesema serikali mpya itakayoundwa itaendeleza mshikamano wa kijamii hiyo na usimamizi bora wa rasilimali.

Naye mgombea udiwani wa kata ya  Oloolosokwan, Methew Mollel, ameeleza kuwa jamii kifugaji ya kimasai inatarajia kupata maeneo ya malisho na kuwekeza katika uhifadhi wa mazingira ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja.

Kwa upande wake, Mbunge Mteule wa CCM wa Jimbo la Ngorongoro Yannick Ndoinyo amewataka wananchi wa Jimbo hilo kumpigia kura nyingi Rais Samia ili aweze kuwatembelea Ngorongoro na kuwapa fedha nyingi za miradi maendeleo katika Jimbo hilo.

Ndoinyo alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya ubunge wake Jimboni Ngorongoro wananchi wake wataweza kujikita zaidi katika biashara na kupunguza utegemezi wa ufugaji pekee.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button