NHIF Mtwara watoa msaada kwa wajawazito

MFUKO wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani Mtwara umetoa msaada wa vifaa vya kujifungulia kwa wajawazito mkoani humo kama sehemu ya mfuko huo kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8 mwaka huu.
Vifaa hivyo vimetolewa leo Machi 6, 2025 katika kituo Cha Afya Cha Likombe , Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Meneja wa mfuko Mtwara, Dk Adolf Kahamba amesema msaada huo umetolea na serikali kupitia NHIF ili kuwapunguzia gharama mama wajawazito wakati wa kujifungua.

“Katika kuandhimisha siku ya wanawake duniani na kwa kutambua umuhimu wa akina mama, mfuko wa NHIF tukaona ni vyema na sisi kuweka alama kwa kuwapatia wamama wajawazito vifaa vya kujifungulia,” amesema.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Dk Elizabeth Oming’o ameshukuru NHIF Mtwara kwa kutoa msaada wa vifaa vya kujifungulia kwa akina mama akisema msaada huo utaleta unafuu kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

“Tunawashukuru sana NHIF mkoa wa Mtwara, wamechagua sehemu sahihi kabisa kutoa msaada huu muhimu sana kwa akina mama wajawazito,” amesema
Dk Oming’o amesema kituo cha afya Likombe kinapokea na kuwahudumia wajawazito zaidi ya 150 kwa mwezi.
“Kituo Cha Afya Likombe kina wateja wengi,kwa sababu kwa wastani tunapokea wajawazito wanaokuja kliniki kwa mwezi ni 150 mpaka 200 na wanaojifungulia hapa ni zaid ya 300 kwa mwezi amesema,”.



