NHIF yafikia ukwasi wa bilioni 95/-

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetengeneza ukwasi wa Sh bilioni 95 mpaka Desemba mwaka jana.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka amesema mafanikio hayo yametokana na kuzuia udanganyifu kwa kiasi kikubwa na matumizi ya Teknolojia ya Habari (TEHAMA) ambayo serikali ya Awamu ya Sita inasisitiza taasisi zake kutumia.
“Kwa serikali ya Awamu ya Sita Mfumo umeondoka kwenye upungufu wa Sh bilioni 120… hii yote ni kutokana na kukabiliana na udanganyifu na kujituma na kubana matumizi kwa watumishi wa NHIF… lakini pia kudhibiti udanganyifu huo tumeokoa zaidi ya Sh bilioni 22 katika kipindi hiki,” alisema Dk Isaka.
Aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dodoma kwamba NHIF imefanikiwa kwenye matumizi ya Tehama kwani mambo mengi yamerahisishwa ikiwemo kusajili wanachama na kupokea taarifa za michango kutoka kwenye vituo ilivyovisajili kwa huduma hiyo.
“Matokeo yake kwa kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, tumesajili wanachama milioni 2.2 na kwa miezi sita, Julai hadi Desemba 2024, tumesajili wanachama 284,543 na tumeongeza ukusanyaji wa michango kufikia Sh trilioni 2.3, kati ya hizo asilimia 92 ni michango ya wanachama, asilimia saba ni pato la uwekezaji na asilimia moja mapato ya vyanzo vingine,” alisema.
“Pia tumeweza kuoanisha taarifa zetu na taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa) ndio maana kwa wale wanachama wetu kwa sasa hata kama huna kadi unaweza kupata matibabu kupitia kitambulisho chako cha Nida,” alisema.
Alisema baada ya kuwa kwenye mfumo wa Tehama, kwa sasa wanatumia siku 45 mpaka 60 kuchakata dai kutoka siku 120 ilivyokuwa mpaka mwanzoni mwa mwaka 2021.
Alisema ulipaji umeongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu vituo vimeongezeka na huduma pia zimeongezeka. Alisema huduma za NHIF zinatambua huduma za magonjwa bobezi kwa wanachama wake.
“Serikali wanapokea asilimia 37 ya madai yote pamoja na kuwa na vituo vingi, binafsi vinapokea asilimia 35 na mashirika ya dini asilimia 28, kwa kipindi cha miaka minne, serikali imelipa zaidi ya Sh trilioni 2.29 kwa vituo vyote, hizo si fedha ndogo na zinazunguka humuhumu nchini,” alisema.
Kwa upande wa wanachama wastaafu ambao kwa sasa hawachangii, alisema malipo yake yameongezeka na mpaka mwaka jana wamelipa Sh bilioni 91 kwa vituo vinavyowahudumia. “Hilo ni eneo ambalo mfuko umeendelea kuboresha,” alisema.
“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yameongezeka sana; sasa hivi kwenye madai yetu, asilimia 60 ya malipo ni tiba ya magonjwa hayo hivyo inamaanisha wanaougua si wazee tu bali hata vijana, tumelipa Sh bilioni 371, ni eneo tunalohitaji sana kutoa elimu kuhamasisha wananchi wafanye mazoezi, kula vizuri kupambana na magonjwa hayo,” alisema.
Alisema mafanikio mengine ya taasisi hiyo ni mikopo waliyotoa kwa vituo inavyofanya navyo kazi na mpaka sasa wametoa mikopo ya Sh bilioni 19.6 kwa taasisi 94. “Mikopo hii ni kwa ajili ya kununua vifaa tiba na kufanya ukarabati wa miundombinu,” alisema.
Alisema kwa sasa taasisi ina mikakati ya kuendelea kuimarisha matumizi ya Tehama ikiwa ni pamoja na kutumia akili mnemba katika mawasiliano kwenye vituo vyake vya huduma kwa wateja.
“Mikakati mingine ni kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la matumizi ya bima ya afya kwa wote, hivyo tutafika kwenye vikundi vyote, mama ntilie, wakulima, wavuvi, wafanyabiashara,” alisema.
Aliongeza: “Lengo la serikali ya Awamu ya sita, kila Mtanzania apate bima ya afya na kwenye hili tumepiga hatua kubwa, mwaka 2023 Rais (Samia) alipitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Agosti 2024 Waziri (Jenista Mhagama) alipitisha kanuni kwa hiyo tumeanza utekelezaji wake.”
Alisema kwa sasa wako kwenye mchakato wa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutambua kaya masikini wazisajili kwa ajili ya bima.
“Ninaposema tunapokwenda kutambua kaya zisizo na uwezo, ni katika hatua hizohizo. Naomba Watanzania tuchangamkie fursa kujisajili bima ya afya maana wengi wanaokuja kukata bima tayari ni wagonjwa, unatakiwa ukate ukiwa na afya ili ukipata dharura upate matibabu,” alisema.
Imeandikwa na Zena Chande (Dar es Salaam) na Magnus Mahenge (Dodoma).



