Doyo ataka uvuvi wa kisasa Kigoma

KIGOMA : MGOMBEA Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, amesema kuwa akichaguliwa kuwa Rais atanunua meli kubwa ya uvuvi ili kufanikisha uvuvi wa kisasa wenye tija katika Ziwa Tanganyika.
Amesema hayo alipohutubia mkutano wa kampeni katika eneo la soko la Buzebazeba, Manispaa ya Kigoma Ujiji, akisisitiza kuwa ziwa hilo bado halijachangia vya kutosha katika mapato ya taifa licha ya kuwa na rasilimali kubwa.
Doyo aliongeza kuwa idadi kubwa ya wavuvi bado wanatumia boti za mbao bila vifaa vya kisasa, jambo linalowapelekea kutumia gharama kubwa huku mapato yao yakibaki madogo. Akisisitiza uhitaji wa kuwekeza katika uvuvi wa kisasa, alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira na mapato kwa wananchi wa Kigoma.SOMA: NLD yaahidi kupitia upya mikataba ya madini
Kwa upande mwingine, mgombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kwa tiketi ya NLD, Hafsa Mussa, amewaomba wapiga kura kumchagua kuwa mbunge pamoja na kuchagua madiwani wengi wa chama hicho. Hafsa alisema manispaa ya Kigoma Ujiji imekuwa nyuma kimaendeleo kutokana na ukosefu wa uongozi wa hali ya juu, huku fedha za umma zikielekezwa vibaya, jambo linalozuia maendeleo ya wananchi.