Noti mpya kuingia kwenye mzunguko Februari Mosi

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania, Emanuel Tutuba amesema noti mpya za Tanzania zenye saini ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na yeye mwenyewe, za toleo la mwaka 2010, zitaingia kwenye mzunguko kuanzia Februari Mosi, mwaka huu.

Gavana Tutuba alisema hayo wakati akimkabidhi, Dk Mwigulu noti kifani za Sh 10,000, 5,000, 2,000 na 1,000 katika ofisi ndogo za Wizara ya Fedha, Dar es Salaam kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazosimamia masuala ya fedha nchini.

“Mheshimiwa waziri, ninayo furaha kukujulisha kuwa uchapaji upya wa noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010, umekamilika na tayari tumewajulisha wananchi kupitia taarifa niliyoitoa kupi[tia Gazeti la Serikali,” alisema Tutuba.

Advertisement

Gavana Tutuba alifafanua kuwa noti hizo zitatumika sambamba na zilizopo sasa na zina mwonekano wa noti zinazotumika hivi sasa zilizotolewa 2010, ikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine. Isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

“Saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango imebadilishwa na ku[1]wekwa saini yako, Dk Mwigulu na saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu, Profesa Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa saini ya Gavana wa Benki Kuu wa sasa, Tutuba,” aliongeza.

Akizungumza baada ya kupokea sampuli za noti hizo mpya, Dk Mwigulu alimshukuru, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika. Alimpongeza, Tutuba kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa. Dk Nchemba aliridhia noti hizo ziingizwe kwenye mzunguko na kuanza kutumika kama ilivyopangwa Februari Mosi, mwaka huu