NRA: Tutashirikisha Diaspora kuinua uchumi

DODOMA: Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Almas Hassan, amesema endapo atachaguliwa kuongoza nchi, ataruhusu Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) wenye uraia pacha kushiriki katika shughuli zote za kijamii na kiuchumi nchini, isipokuwa kugombea nafasi ya urais.

Akizungumza na Daily News Digital, Almas amesema hatua hiyo inalenga kutumia elimu, ujuzi na teknolojia waliyonayo diaspora kutoka mataifa wanayoishi ili kuleta maendeleo ya taifa.

Amesema kwa muda mrefu Tanzania imekuwa na mashaka kuhusu kuwapa nafasi diaspora, kwa hofu kuwa wanaweza kuchukua nafasi za watu waliopo nchini, jambo ambalo linakwamisha maendeleo.

Almas amesema serikali yake itaweka sheria maalum zitakazowawezesha Watanzania hao kutumia ujuzi wao katika sekta mbalimbali kama vile elimu, afya, teknolojia, biashara na utafiti, lakini haitaruhusu wao kugombea nafasi ya urais ili kulinda misingi ya uraia wa kizalendo.

Katika hatua nyingine, Almas amesema serikali inapaswa kuandaa mifumo ya kuwawezesha wananchi kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa. Ameeleza kuwa mifumo hiyo lazima izingatie haki na usawa ili kila Mtanzania apate nafasi sawa ya kujikwamua kiuchumi.

Kuhusu uchaguzi, Almas amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao huku wakilinda amani ya nchi, huku akiwashauri wanasiasa kuacha kutumia kauli zenye viashiria vya uchochezi kama vile “piga kura, linda kura”, akisema kauli hizo zinazua hofu na taharuki kwa wananchi.

Almas amesisitiza kuwa uchaguzi ni sehemu ya demokrasia, hivyo unapaswa kufanyika kwa amani na utulivu ili taifa liendelee kusonga mbele.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button