NRA yaahidi kuanzisha wizara mambo ya hovyo

DODOMA: Mgombea urais kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Hassan Almas, amesema endapo chama chake kitapata ridhaa ya kuongoza nchi, kitaanzisha Wizara Maalum ya Kudhibiti mambo ya hovyo ikiwemo rushwa, matumizi mabaya ya ofisi, wizi wa mali za umma na uzembe kazini.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Daily News Digital, Almas amesema hatua hiyo inalenga kukabiliana na upotevu wa fedha za umma unaobainishwa kila mwaka katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Sisi katika Wizara kumi tutaweka Wizara moja ya kudhibiti masuala yote ya hovyo kama rushwa, wizi, uzembe na uvuvi. Ukisoma ripoti ya CAG miaka yote, shida kubwa ni upotevu wa fedha za nchi upo katika uzembe na matumizi mabaya ya ofisi, sasa sisi hayo mambo tutayaanzishia Wizara” amesema Almas.
Amesema Wizara hiyo itakuwa na idara mbili kuu; Idara ya Maadili na Idara ya Mambo ya Rushwa, ambazo zitahakikisha kila mtumishi wa umma anawajibika kulingana na matendo yake kazini.
Aidha, Almas amekosoa tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali kusafiri na wasanii katika shughuli mbalimbali, akisema kuwa ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma, huku akisisitiza kuwa mali za umma zinapaswa kutumika kwa manufaa ya wananchi wote, si kwa maslahi binafsi ya viongozi.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo amewataka wagombea wenzake kuacha tabia ya kutoa ahadi zisizotekelezeka kwa wananchi wa vijijini, akisema ni vema kutoa ahadi zenye uhalisia na zinazotekelezeka.



