NYANI: Wanyama ‘wanaoabudu ndoa za mitala’

“WANYAMA hawa (nyani) asubuhi wanapoamka kabla ya kuanza majukumu yao, ni lazima kwenda kumsalimia dume ambaye ni kiongozi wa familia kwa kumkumbatia ingawa hawakosekani wababe wengine wanaoitamani nafasi yake kwa sababu ana uwezo wa kuwa na jike yeyote ndani ya kikundi ambaye yuko tayari kuzaliana.”
Unaandika ukurasa wa Facebook wa Antomatv mtandao Julai 14, 2021 chini ya kichwa cha habari: ‘Fahamu Tabia za Kuvutia za Nyani’ na kuongeza: “Hata hivyo, ugomvi kwa madume kuonesha uwezo wao ili waweze kumtoa ni karibia kila siku.”Unasema: “Wapo wezi pia wasioweza kugombana, bali wanapata jike kutokana na kuwasaidia majike kulea watoto wao na kuonesha kuwajali zaidi ingawa hii hufanyika kwa siri bila mwenye nafasi kujua.”
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, nyani ni kiumbe mwenye ufanano wa mambo mengi na binadamu. Hata hivyo vinasema pamoja na ufanano huo, nyani ana tofauti kubwa na mwanadamu na kubwa zaidi ni kwamba, binadamu ana ufahamu timamu wa kuratibu na kujiongoza katika mambo mazuri na mabaya, wakati kwa viumbe wengine wote wakiwamo wanyama lakini nyani hawana bahati hiyo.
Ifahamike kwamba nyani ni miongoni mwa viumbe ambao hufanana sana na viumbe wengine wa jamii yake, kiasi kwamba viumbe hao nao huitwa nyani, wanyama ambao hufananishwa na nyani ni pamoja na sokwe, mbega, tumbiri na jamii zote za kima pamoja kuwa na majina yao hayo lakini binadamu awaonapo huwaita nyani.
Februari 6, 2019, Kanungila Karim katika ukurasa wa Jamii Forum chini ya kichwa cha habari: ‘Wafahamu Nyani! Wanyama Wanaoamini Sana Katika Mitala’ aliandika kuhusu nyani. Katika chapisho hilo anasema, nyani wawapo katika makazi yao huishi kwa familia na hutengeneza uongozi wao ambao huheshimiwa.
“Watakuwepo walinzi, wawindaji pamoja na viongozi wakuu wa kitaifa ambao ndio hufanya maamuzi pindi linapotokea jambo la kuamriwa… “Viumbe hawa ni waumini wazuri wa demokrasia na hufanya maamuzi kwa kukubaliana na endapo miongoni mwao watakuwepo ambao wanapingana na maamuzi hayo, basi jukumu lao huwa ni kuondoka katika utawala huo na kwenda kuanzisha makazi yao mapya,” anaandika.
Karim katika chapisho lake anasema wapo pia nyani ambao ni watukutu hususani madume hasa vijana, ambao mara kadhaa hujaribu kutaka kufanya mapinduzi katika utawala unaokuwepo, yanapofanikiwa hushika dola, lakini yakishindwa ‘hukiona cha mtema kuni.’
Chapisho linasema: “Nyani pia ni viumbe ambao wanaamini sana katika mitala, ni jambo la kawaida sana dume kumiliki majike zaidi ya watatu. Mbali na mfumo huo, pia ni viumbe ambao wanaamini sana katika mfumo dume.
“Jike ndiye huwa na hatimiliki ya watoto, hivyo anapopata majukumu ya kufanya kuliko ampeleke mwanaye kwa dume lake, huwa tayari amuachie mwanaye rafiki yake. Jike la nyani katu haliwezi mkabidhi mwanaye kwa mke mwenza kwani historia zao za uke wenza huanzia kwenye urafiki tu.
Kwa mantiki hiyo, wake wenza wote huwa ni sehemu ya adui zake… Endapo mtoto wake huyo atakuwa dume siku atayopevuka jike atapewa na dume ambalo ndilo litakuwa linaongoza kaya hiyo na si vinginevyo.” Kwa umbo, vyanzo mbalimbali vinasema jike huwa mdogo kwa dume na urefu wake jike mkubwa huwa sentimeta 60 sawa na rula mbili na dume huwa na sentimeta 70.
“Kwa uzito,” chapisho hilo mtandaoni linasema: “Madume huwa zaidi pia hufikia mpaka kilo 60 na zaidi, jike hupevuka afikishapo miaka 5 mpaka 7 na hudumu na mimba kwa miezi 6, mpaka atakapozaa mtoto wake mmoja.
“Nyani hawa huishi kwa miaka zaidi ya 25, chakula chao kikuu huwa nafaka na nyama, hivyo ni wanyama wa kundi la kati ambao hula mimea na nyama.”
Chanzo kinasema chakula chochote anachokula mwanadamu nyani pia huweza kukitumia. Kwamba, katika kundi la nyama, nyani hupendelea samaki, kuku, sungura, panya, mbuzi, kondoo na kwa upande wa nafaka, wanyama hawa hula karanga, mtama, mahindi, ulezi na matunda takribani yote yanayotumiwa na binadamu mfano, ndizi, tikiti, embe, nanasi na mengine.
Julai 10, 2018 Tovuti ya Mkoa wa Mbeya iliandika makala yenye kichwa cha habari: ‘Mjue Nyani Kipunji Kutoka Hifadhi za Mlima Rungwe’ ikisema nyaki aina ya kipunji (nyani kipunji) anakula vyakula vya aina tofauti yakiwepo majani machanga na yaliyokomaa, maua, matunda mabichi na yaliyoiva na mazao ya shambani kama mahindi na viazi.
Wanyama hawa wanatajwa kuwa na sifa kadhaa nyingine zikiwa zinazofanana na bnadamu kwa mfano, kama ilivyo kwa binadamu, nyani pia huwinda wanyama kwa ajili ya chakula na isivyo bahati kwao, nyani wakubwa hula nyani wadogo ili mradi tu, wawe ni wa jamii tofauti.
Chapisho moja mtandaoni linasema nyani ni wanyama waharibifu kama walivyo tembo, kiboko na baadhi ya ndege ambao huvamia mashamba ya binadamu na kufanya balaa na pia, wanyama hawa wanapohitaji nyama kama ya mbuzi au kondoo, huvamia makazi ya binadamu.
Linasema: “Silaha zake kubwa ni mbili; hunasa makofi na usiombe upatwe na kofi lake shubiri yake mbwa wa wawindaji huifahamu, silaha ya pili ni meno akipitisha sehemu anararua.” Chapisho linaongeza: “Jike hubeba mtoto mgongoni au tumboni. Wanapotembea huwa katika makundi makubwa makubwa na huwasiliana kwa kunguruma na kutoa sauti kama ya kubweka pindi wanapohisi hatari.”
Kuhusu uaminifu katika suala la mapenzi na ndoa, Karim katika chapisho lake anaandika: “Ni viumbe wasio waaminifu katika mapenzi kwani pamoja na kumiliki majike zaidi ya mmoja na majike kumilikiwa, bado huwa na uhusiano wa kimapenzi na mwenzie yoyote nje ya kambi yao.”
Linaongeza: “Ni viumbe ambao wanapokutana kimahaba jike na dume huweza kutekeleza mahaba yao kwa kiasi na ufundi ule ule ambao binadamu huutumia, wakitaka watizamane, wasionane inawezekana tu. Huweza kufanya vitu vingi afanyavyo mwanadamu ikiwa ni pamoja na kuruka sarekasi, kucheza, kuoneshana mahaba, kukimbizana nk.”
Uchunguzi wa gazeti la HabariLEO umethibitisha kuwa, nyani awapo katika hali mbaya (hatari) hutia huruma na hiyo ndiyo sababu ya msemo wa Kiswahili kuwa: “Ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni,” maana utamhurumia na kumsamehe hata kama ameharibu shamba zima.
Nyani ana njia mbili kuu za kuachana na mwanaye ili nyani mdogo akajitegemee. Njia ya kwanza kwa mujibu wa chanzo, ni kusubiri mpaka nyani mtoto anapoonesha dalili zote za kupevuka na namna ya pili, ni kupitia majaribio ya mara kadhaa kutaka kujua amefikia wapi.
Katika hili chanzo kinasema, nyani (mama) huchukua nafaka na kuchanganya na mchanga kisha humpa mtoto wake. Kosa atakalofanya mtoto huyo ni kama atajaribu kutaka kutenganisha mchanga na nafaka hizo maana hapo, mama yake atapiga mpaka mtoto akimbie na akikimbia tu, kuanzia siku hiyo wanakuwa wameachana.
Kwa mujibu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), nyani kipunji waliogunduliwa mwaka 2003 katika Mlima Rungwe na maeneo mengine yanayoizunguka milima hiyo tu, aligunduliwa na Shirika la Kimataifa la Hifadhi ya Mazingira na Viumbe hai (WCS) mwaka 2003 ni moja kati ya hifadhi za asili ambazo ni rasilimali pekee ya Taifa zinazohitaji kutunzwa mazingira yake.
“Nyani kipunji kuwa ni mnyama mwenye aibu ambaye kumuona kwake kunahitaji tahadhari na inawezekana kwa siku mbili au tatu asionekane ingawa kuna wakati hutembea kwa makundi… Anakula vyakula vya aina tofauti yakiwepo majani machanga na yaliyokomaa, maua, matunda mabichi na mazao ya shambani kama mahindi, viazi nk,” inasema TSF katika akaunti yake ya Facebook chini ya chapisho la Machi 14, 2021 lenye kichwa cha habari: ‘Mjue Nyani Kipunji Kutoka Hifadhi za Mlima Rungwe.’
Juni 20, 2022 gazeti moja litolewalo kwa Kiswahili kila siku nchini liliandika mtandaoni kuwa, kundi la nyani wa Hifadhi ya Gombe iliyopo kijijini Mwamgongo, Kigoma limevamia nyumba ya Shayima Faya (20) na kumpokonya mtoto mchanga wakati akimnyonyesha na kutokomea naye.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, james Manyama alisema tukio hilo lilitokea Juni 18, 2022 kijijini hapo. Alisema juhudi za wananchi kuwakimbiza nyani hao ziliwezesha kupatikana mtoto huyo akiwa amejeruhiwa na akafariki dunia baada ya kufikishwa katika Kituo cha Afya cha Mwamgongo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti la HabariLEO, nyani ni miongoni mwa wanayamapori wanaovutia kutokana na tabia zao na mara nyingi, huonekana katika makundi makubwa hata katika malango ya kuingilia hifadhi mbalimbali, ikiwamo Hifadhi ya Ngorongoro iliyopo Arusha.



