Nyenzo ya kuchochea maendeleo ya kilimo – biashara

MAONESHO ya Nane Nane hufanyika kila mwaka kuanzia Agosti, Mosi na kufikia kilele Augosti 8, yakiwa ni sehemu ya kuadhimisha na kutambua mchango wa wakulima na wafugaji katika maendeleo endelevu wa kukuza uchumi wa Tanzania.
Maonesho hayo ya wakulima, kimsingi yalianza miaka ya 1960, yakilenga kutambua mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa na yalikuwa yakiadhimishwa kama Sabasaba, Julai 7 kila mwaka.
Kutokana na Mabadiliko ya Kisera ya Mwaka 1977, maonesho ya wakulima yalipewa msukumo mkubwa kupitia Sera ya Siasa ni Kilimo, ambapo wakulima walihamasishwa kuonesha mazao na teknolojia za kisasa.
Miaka ya 1990, serikali ilibadilisha rasmi tarehe ya maonesho haya kuwa Agosti 8, na kuifanya siku hiyo kuwa Sikukuu ya Wakulima pekee na ile ya Julai 7, kwa maana ya Sabasaba ikibaki kuwa ya wafanyabiashara. Kutokana na kuwepo kwa mwendelezo mzuri ya maonesho hayo ya Nanenane mwaka 1993, yalianza kufanyika kwa mtindo wa kanda yakihusisha mikoa mbalimbali ili kuwafikia wananchi hususani wakulima wengi zaidi.
Tangu kuanzishwa mwaka 1993 kwa mtindo wa kikanda, maonesho haya yameendelea kuvutia maelfu ya washiriki wakiwemo kutoka taasisi za utafiti, mashirika ya maendeleo, kampuni za zana za kilimo na wakulima na wafugaji.

Maonesho haya yamekuwa jukwaa muhimu kuhamasisha mabadiliko ya sekta ya uzalishaji kupitia teknolojia, elimu na ubunifu unaowafikia wakulima, wafugaji na wadau wa kilimo katika maeneo yao. Kimsingi, maonesho ya wakulima huchochea ushirikiano wa karibu kati ya wakulima, wafugaji, wajasiriamali na taasisi za kifedha.
Hadi sasa Maonesho ya Nanenane hufanyika katika Kanda ya Kati inashirikisha mikoa ya Dodoma na Singida hufanyika kwenye Uwanja wa Nzuguni uliopo mkoani Dodoma. Kanda ya Mashariki yenye mikoa ya Morogoro, Pwani, Tanga na Dar es Salaam na yanafanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere mkoani Morogoro.
Nyingine ni Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayohusisha mikoa ya Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Njombe ambayo hufanya maonesho hayo katika Uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya. Ipo pia Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Lindi na Mtwara.
Maonesho ya Kanda hiyo hufanyika katika Uwanja wa Ngongo mkoani Lindi na kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yenye mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera hufanyika uwanja wa Nyamhongolo, Mwanza. Nyingine ni Kanda ya Ziwa Mashariki ambayo inashirikisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga na kufanyika katika uwanja wa Nyakabindi mkoani Simiyu.
Maonesho haya pia hufanyika katika Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro na kufanyika katika uwanja wa Themi uliopo mkoa wa Arusha. Kanda nyingine ni ya Magharibi ambayo inayojumuisha mkoa wa Tabora, Kigoma na Katavi. Maonesho ya kanda hiyo hufanyia katika uwanja wa Fatuma Mwasa mkoani Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima anasema mwaka huu Tanzania inaadhimisha Maonesho ya 32 ya Nane Nane ambayo yamebeba dhima ya hadhi ya kimataifa yakivutia washiriki wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi. Maonesho hayo ambayo mwaka huu yanaongoizwa na kaulimbiu: ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo elimu na teknolojia mpya kwa wakulima na wafugaji.
Anasema maonesho ya Nanenane si tu sikukuu ya wakulima na wafugaji, bali ni jukwaa linalochangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia ubunifu, elimu na ushirikiano.
Malima anasema Watanzania hususani wakulima na wafugaji hujifunza njia bora za kuboresha sekta za uzalishaji na kuongeza ajira, tukio la kimkakati lenye mchango chanya unaogusa sekta mbalimbali kutoka vijijini hadi mijini.
Anasema Maonesho ya Nanenane hutoa fursa kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali kuonesha bunifu, kujifunza teknolojia mpya na kushirikishana uzoefu ili kuongeza tija na uzalishaji ikiwa ni pamoja na kuchochea maendeleo ya kilimobiashara na ajira kwa vijana.

Malima anasema kwa Kanda ya Mashariki itaendelea kubeba maono ya kukuza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini kutokana na jiografia ya mikoa yake kuwa na ardhi nzuri na yenye rutuba katika uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali na ufugaji bora.
Kwa mujibu wa Malima, mikoa ya Morogoro, Tanga, Dar es Salaam na Pwani ina jukumu kubwa la kuzalisha kwa wingi mazao yatakayowezesha utoshelevu wa chakula na ziada pamoja na malighafi za viwandani. “Mfano mzuri, Mkoa wa Morogoro unasimamia uendelezaji wa mazao ya kimkakati yakiwemo karafuu, kakao, parachichi na kahawa, ambayo yatachochea ukuaji wa uchumi ndani ya Mkoa na Taifa kwa ujumla,” anasema Malima.
Kuhusu ufugaji, Malima anawasisitiza kwa wafugaji kufuga kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya sasa na kuacha ule ufugaji wa mifugo mingi isiyo na tija kwao. Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Devotha Mosha anaeleza namna walivyojipanga katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki mwaka huu ni pamoja na kuonesha teknolojia mpya za aina mbalimbali.
Dk Mosha anataja teknolojia hizo mpya ni pamoja na za kilimo, misitu, masuala ya ugani na namna ya kutibu mifugo mbalimbali. Anawakabirisha wakulima, watafiti, maofisa ugani wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na wanafunzi kutembelea banda la chuo kikuu hicho kuangalia na kujifunza teknolojia mpya ambazo Sua kinazizalisha.
“Sua tumejipanga vyema maonesho ya mwaka huu na tunawakaribisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Mkoa wa Morogoro waje wajionee wenyewe teknolojia hizi mpya ambazo Sua imeziandaa,” anasema Mosha. Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishajimali wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rozalia Rwegasira anasema Maonesho ya Nanenane huleta bunifu na teknolojia mpya kwa makundi ya wakulima na wafugaji.
Anasema maonesho hayo ni fursa muhimu kwa wakulima na wafugaji kujifunza kwa vitendo jambo linalosaidia kubadilisha kilimo cha mazoea na ufugaji wa kizamani pamoja na kutoa elimu ya kuimarisha mnyororo wa thamani ya mazao.
Anasema elimu hiyo inawajengea uwezo wa huongeza mapato na kupunguza upotevu wa mazao, pia kuchochea uanzishwaji wa viwanda vidogo vijijini vinavyotumia malighafi itokanayo na sekta ya kilimo na
mifugo.
Meneja wa Uwanja wa Nanenane Kanda hiyo na Ofisa Mazingira, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Venance Segere anasema mwaka huu wameandaa kuwa na jukwaa maalumu la kutoa mafunzo ya kilimo na biashara kwa wananchi.
Mafunzo hayo yanatarajia kutolewa na wataalamu mbalimbali wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi wakati wa maonesho ya wakulima na wafugaji (Nanenane) Kanda ya Mashariki yatakayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuanzia Augosti Mosi, 2025.
Meneja huyo anasema wakulima na wafugaji zaidi ya 700 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo maalumu ya kilimo kinachozingatia tija, ufugaji bora wa mifugo na samaki ili kukuza vipato vyao kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Segera anasema mada mbalimbali zitatolewa katika mafunzo hayo kwa washiriki kuanzia Augosti 2 hadi siku ya kilele Augosti 8, mwaka huu ambapo watu zaidi ya 700 watanufaika na mafunzo hayo kuhusu kilimo bora, ufugaji wa kisasa na masuala ya kilimo biashara.
“Kuanzia Augosti 2 hadi Agosti 8 ambayo ni siku ya kilele cha Maonesho ya Nanenane kila siku tunatarajia kuwa na wananchi 100 watakaopata mafunzo kupitia mada zitakazotolewa kuanzia saa nne asubihi hadi 10 jioni,” anasema Segere na kuongeza kuwa, mafunzo hayo yatahusisha mada zitakazowezesha wakulima na wafugaji kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi.
Anataja baadhi ya mada zitakazotolewa kuwa ni pamoja na afya ya udongo, mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa mazao stakabadhi ghalani. Nyingine zitahusisha masuala ya kodi, usindikaji wa mazao, uvunaji wa mazao unaozingatia udhibiti wa upotevu na uhifadhi bora wa chakula.



