TANGA: Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Said Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi watatu na kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili ikiwemo kuongeza gharama za ujenzi wa miradi ya halmashauri kutoka Sh milioni 584.2 hadi kufika Sh milioni 702 tofauti na maelekezo.
Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kukagua ujenzi wa shule ya sekondari ya Kiomoni ambayo inajengwa kupitia mradi wa SEQUIP ambapo alisema kuwa watumishi hao wamekiuka na kuongeza gharama za ujenzi na kusababisha mradi kutokamilika kwa wakati.
Amewataja watumishi hao kuwa ni Kaimu mkuu wa Idara ya ujenzi na Miundombinu Issa Mchezo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kiomoni, Fredrick Lubangulila pamoja na mhandisi wa majengo wa halmashauri, Baraka Sylivester.
Alisema kuwa serikali ilitoa kiasi cha sh milioni 584.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo mpya ya kata lakini kutokana na kuongeza gharama za ujenzi huo umepelekea hadi gharama za ujenzi kuongezeka na kufikia Sh milioni 702.
“Shule hii ilitakiwa iwe imemalizika mfano jengo la utawala maelekezo ni lijengwe kwa Sh milioni 77.7 lakini mhandisi ametengeneza BOQ ya Sh milioni 140 na mkuu wa shule na kamati yake wakaruhusu na kutoa mkataba na ujenzi uanze”alisema DED Majaliwa.
Aidha akitolea mfano wa ujenzi wa majengo ya maabara shuleni hapo bajeti iliyoelekezwa na wizara ilikuwa ni Sh milioni 102 lakini gharama iliyotumika ni Sh milioni 150 kinyume na maelekezo yaliyotolewa.
Mkurungenzi huyo alisema kuwa kutokana na gharama za mradi kuongezwa kumesababisha majengo mengine katika mradi huo wa shule kutojengwa kutoka na fedha kumalizika.
Aliyataja majengo mengine ambayo yalitakiwa yajengwe kwenye mradi huo lakini hayajengwa kuwa ni maktaba, chumba cha Tehama pamoja na matundu ya vyoo.