Nyumba 155 zaunganishwa gesi asilia Mikocheni Dar

DODOMA – NYUMBA 155 zimeunganishwa na mtandao wa matumizi ya gesi asilia katika eneo la Mikocheni, Dar es Salaam na kuwa mpango wa sasa ni kuendelea kuunganisha nyumba zaidi ya 1,000.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula aliliambia bunge jana mjini hapa wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbas (CCM), aliyehoji serikali imefikia wapi katika mradi wa kusambaza gesi ya kupikia nyumbani wilayani Kinondoni.

Akijibu, Kitandula alisema katika Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam serikali imeshapeleka miundombinu ya usambazaji gesi asilia ambapo nyumba 155 zimeunganishwa na mtandao wa matumizi ya gesi asilia katika eneo la Mikocheni.

Pia, serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC) ipo katika mpango wa kuunganisha nyumba zaidi ya 1,000 katika maeneo ya Dar es Salaam ambapo kati ya nyumba hizo, nyumba 279 zipo wilayani humo.

Katika swali lake la nyongeza, Tarimba alisema mradi huo wa kusambaza gesi nyumbani ulianza Januari 2021 na lengo ilikuwa kuzifikia nyumba zaidi ya 170 na kuwa leo ni miaka mitatu imepita na nyumba zilizounganishwa ni 150.

Alihoji ni lini sasa serikali itakamilisha nyumba zilizobaki kuunganishwa na nishati hiyo.

Akijibu, Kitandula alisema ni kweli mpango ulikuwa huo lakini maombi yaliyopokelewa ya wateja yalikuwa mengi na serikali ikachukua hatua ya kuingia makubaliano na Kampuni ya TAQA Dalbit ili kusambaza nishati hiyo.

Kuhusu hoja kuwa gesi ikiisha mteja hupelekewa namba ya malipo na akishalipia lazima apige tena simu TPDC kufunguliwa gesi na kusema mfumo huo una changamoto na kwa nini wasitumia mfumo kama wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Akijibu hoja hiyo, Kitandula alisema ni kweli wamepata malalamiko hayo na sasa timu ya wataalamu wao iko kazini, wanaangalia mfumo mzuri utakaotatua changamoto hiyo.

Mbunge wa Meatu, Leah Komanya (CCM) katika swali lake la nyongeza alihoji kwa nini mitungi ya gesi inayotolewa katika jimbo hilo isitolewe kwa utaratibu wa kaya badala wa kutumia Kitambulisho cha Taifa (NIDA).

Alisema utaratibu wa sasa ni kuwa kila mwenye kitambulisho anapewa gesi hiyo ya mtungi mdogo kwa bei ya Sh 20,000 na kusema mfumo huo si rafiki kwa sababu kaya moja inaweza kupata mitungi zaidi ya mitano na kaya nyingi kukosa.

Lakini ukitumika utaratibu wa kutoa gesi hiyo kwa kaya, ni wazi kuwa kaya nyingi zitanufaika na nishati hiyo safi. Akijibu, Kitandula alisema wamepokea ushauri huo na wanakwenda kuangalia jinsi ya kuyafanyia kazi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button