NYUMBU: Uhamaji na uwezo ‘kushikilia mimba’ siku 90 bila kuzaa

NYUMBU ni wanyamapori wanaopatikana kwa wingi katika mbuga na hifadhi mbalimbali nchini.

Hawa ni wanyama wanaodhaniwa na baadhi ya watu kuwa hawana akili, lakini si kweli kwamba hawana akili ndio maana wanazaa, wanatunza na kulinda watoto. Hata hivyo, baadhi ya wengi wanaamini kuwa, nyumbu ni wanyama wepesi kusahau.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, moja ya maajabu ya wanyamapori hawa ni kwamba, nyumbu wa kike huwa wote wanapandwa kwa wakati mmoja tu kwa mwaka na katika eneo maalumu na wote hushika mimba kwa pamoja katika kipindi hicho.

Chanzo kimoja kiliandika mtandaoni kuhusu mnyamapori huyu kikisema: “Yaani ni mahali maalumu kama chumba cha baba na mama.” Kinaongeza: “Hivyo kabla muda wa kupandwa haujafika, maelfu kwa maelfu ya nyumbu hutoka mbio kutoka nchini Tanzania katika Mbuga ya Serengeti na kuhamia katika Mbuga ya Masai Mara nchini Kenya kwenda ‘kutengeneza watoto’.”

Safari hiyo huanzia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hadi Masai Mara nchini Kenya, kabla ya msafara huo kurejea tena nchini Tanzania.

Akihutubia kikao cha pamoja cha Bunge la Seneti na Bunge la Kitaifa nchini Kenya, Mei 4, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia uhusiano baina ya Kenya na Tanzania akiuhusisha na asili ya wanyama hao akisema: “Ushirikiano wa Tanzania na Kenya si wa hiari.”

Akaongeza: “Wanyamapori (nyumbu) wanakuja hapa Kenya kupata mimba kisha wanarudi kuzaa Tanzania. Kama Wanyama wana udugu, sisi wanadamu tunatengana wapi.” Kimsingi, tukio hilo la uhamaji wa nyumbu hujulikana kwa jina maarufu la ‘Serengeti Migration’ na ni kivutio kikubwa kwa watalii kutoka pembe nne za dunia kukusanyika Serengeti, kushuhudia tukio hilo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa ikolojia ya eneo la Serengeti, nyumbu na wanyama wengine, huzunguka katika ikolojia hiyo kwa zaidi ya kilomita 1,000 kila mwaka na kufanya mzunguko huo kuwa wa kipekee.

Hata hivyo, chanzo cha moja ya maajabu haya ya asili duniani ni eneo la Ndutu lenye kilometa za mraba zaidi ya 8,000 likijumuisha sehemu ya Kreta ya Ngorongoro, Olduvai Gorge ambayo ni chimbuko la historia ya zamadamu na sehemu ya hifadhi ya Serengeti.

Katika makala aliyoandika katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forum Februari 24, 2027 yenye kichwa cha habari: ‘Maajabu ya Nyumbu na Uwezo wa Kuihifadhi Mimba Iliyokomaa Kwa Siku 90 Kusubiria Mazingira Wezeshi’ mwandishi Pascal Mayalla anazungumzia ‘Chumba cha baba na mama’ kwa nyumbu.

Anasema: “Ni eneo dogo linaloitwa Ndutu ambapo nyumbu zaidi ya milioni moja hukutana hapo mwezi Februari na hukaa na ujauzito kwa miezi 11, kisha hurudi eneo hilo hilo kuja kujifungulia hapo na kunyonyesha mtoto kwa mwezi mmoja tu, kupokea mimba nyingine na kuondoka eneo hilo hadi mwaka unaofuata.”

Mwandishi huyo anasema ndivyo inavyakuwa kwa miaka yote, lakini kwa mwaka 2017, hali ilikuwa tofauti kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha ukame. Kwamba, kundi kubwa la nyumbu wenye mimba walikusanyika eneo la Ndutu wakisubiri kujifungua na kutengeneza watoto wapya, lakini kutokana na hali ile ya ukame hakukuwa na majani mabichi machanga.

Anasema katika chapisho lake: “Miili ya nyumbu hao wenye mimba kubwa zilizokomaa, imeweka zuio la muda kuzuia watoto kuzaliwa kwa kusubiria kwanza mpaka mvua zinyeshe, majani mabichi machanga yaote ndipo miili hiyo iruhusu watoto wazaliwe.”

Makala ikamnukuu aliyekuwa Ofisa Uhusiano wa Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Pascal Shelutete akisema nyumbu hao wana uwezo wa ‘kushikilia mimba’ tumboni mwao hadi siku 90.

Katika moja ya makala zake katika TRT-Afrika mtandaoni akiwa Instanbul nchini Uturuki, Edward Qorro anaandika kuwa, safari ya wanyama hao huanzia kati ya Februari na Machi kila mwaka na hutanguliwa na hatua ya kuzaliwa kwa nyumbu katika eneo la Ndutu.

Kwamba, nyumbu wana uwezo wa kuahirisha zoezi la kuzaa kwa sababu za kiusalama kwa watoto wao na uhakika wa chakula na maji. “Nyumbu wengi huzalia katika eneo la Ndutu kutokana na uhakika wa maji na chakula unaopatikana hapo,” anaandika.

Makala inaongeza: “Majani ya eneo hilo yana madini ya kutosha yenye ‘phosphorous’ (fosferasi), ‘calcium’ (kalisi) na ‘magnesium’ (maginesi) na ndio maana nyumbu akidondosha tu mtoto, haichukui muda mrefu kabla hajaanza kutembea mwenyewe.”

“Kinachoimarisha misuli ya miguu ya nyumbu hao wadogo ni maziwa yanayotokana na majani yenye virutubisho hivyo. Baada ya kuzaliwa, safari ya uhamaji wa nyumbu hao huanza, kutafuta malisho na maji.”

Changanoto katika msafara
Inaelezwa kuwa, wanapokuwa katika uhamaji wao, nyumbu hukutana na wanyama wakali wakiwamo simba, chui na fisi na hivyo, wengine kushambuliwa na kuuawa.

Uchunguzi kupitia vyanzo mbalimbali unabainisha kuwa, hata wakati wa kuvuka maji yaendayo kasi ya Mto Mara, nyumbu hukutana na changamoto za kiusalama kwani hushambuliwa na mamba, viboko na wakati wengine baadhi kusombwa na maji.

Kimsingi, moja ya vivutio vinavyolifanya eneo la Serengeti kuwa la kipekee, ni tukio la uhamaji wa nyumbu. Serengeti imeibuka kama hifadhi bora kabisa Afrika kwa mara ya tano mfululizo. Chanzo kimoja ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kinabainisha kuwa, kwa kawaida nyumbu hao wapo katika eneo la Ndutu ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Kinasema hilo ni eneo la tambarare lenye miti midogo na malisho mengi na ndipo wanyama hao huzaliana zaidi kabla ya kuingia Serengeti na kuvuka Mto Mara kwenda Masai Mara nchini Kenya katika miezi ya mvua ya kuanzia Machi hadi mvua zinapokaribia Agosti hadi Septemba wanapoanza kurudi kupitia Loliondo.

Vilevile chanzo kinaeleza: “Nyumbu wana tabia moja ya kipekee kwamba, kama hali ya hewa hairidhishi na ni kipindi cha malisho kidogo, wana uwezo wa kuahirisha kuzaa na wakakaa na mimba iliyo tayari kuzaliwa hata kwa miezi miwili hadi mitatu kusubiri malisho. Mzunguko huo kama wa saa ni ikolojia muhimu ukiiharibu umeharibu mfumo mkubwa wa wanyapaori”.

Chanzo kinasema: “Mfumo wa Ikolojia wa Serengeti Mara-Ngorongoro hutegemea uhamaji wa kila mwaka wa wanyama hao wapatao milioni 1.6 (nyumbu).” Kinaongeza: “Mto Mara ndio chanzo pekee cha maji katika Serengeti ambacho kinaweza kuendeleza uhamaji mkubwa wakati wa kiangazi.”

“Iwapo mto utakauka kwa sababu ya mabwawa na ukataji miti katika sehemu ya juu ya mto huo, litakuwa janga kubwa ambapo takribani nyumbu 500,000 wanaweza kufa katika mwaka wa kwanza.”

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, nyumbu hubeba mimba kwa siku takribani 260 hivi na mtoto wa ndama anayezaliwa wakati huo, anaweza kutembea ndani ya dakika 3 na hadi kufika dakika 30, anaweza kushiriki na kufanya uhamaji huo wa nyumbu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button