Nzilanyingi kushughulikia kero za mafuriko

MBUNGE wa Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza, John Nzilanyingi, amefanya ziara katika Kata ta Mirongo kusikiliza kero za wananchi, akaelezwa pamoja na mambo mengine, uchakavu na ufinyu wa mto mirongo unavyosababisha mafuriko katika kila msimu wa mvua, hatimaye kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii.

Akiwa Mtaa wa Misheni, wananchi wanaofanya biashara ya kuuza mapipa katika daraja la Uhuru unapopita mto huo wamedai kuathirika zaidi, kiasi cha bidhaa zao kusombwa na maji.  “Hali hii inaathiri mitaji yetu, lakini pia tunakuwa hatufanyi biashara kwa uhuru,” ametoa maoni yake mmoja wa wafanyabiashara, Hadiso Msoud.

Katika eneo la daraja la wamasai, maarufu daraja la ‘wakoma’, Nzilanyingi ameelezwa kero hiyohiyo, wananchi wakadai barabara kutopitika kabisa mvua zikinyesha, kutokana na daraja hilo kujaa maji. Wametoa kero pia ya baadhi ya barabara kukosa alama muhimu, hasa ya pundamilia, hatua inayosababisha ajali za mara kwa mara. “Lakini pia taa za barabarani hazifanyi kazi, tunahitaji kufahamu zimewekwa kama mapambo au zinapaswa kuwaka,” amehoji mwananchi Emmanuel Magesa.

Mbunge huyo amewahakikishia wananchi kwamba kero zote zitaisha muda si mrefu, hasa upanuzi wa mto Mirongo unaotarajia kuanza wakati wowote, kwani serikali tayari imetenga fedha kwa ajili hiyo. Meneja wa Wakala wa Barabara za mijini na vijijini (Tarura), Mhandisi Danstan Kishaka, amethibitisha ukarabati huo kuanza mwezi huu katika daraja la wakoma, na unatarajia kukamilika mwezi Aprili, mwaka huu. SOMA: Serikali kujenga kiwanda cha chakula cha samaki Mwanza

Akizungumzia taa za barabarani, Mhandisi amekiri baadhi yake kutofanya kazi, chanzo kikubwa kikiwa ni baadhi ya wananchi kuiba betri zake. Pamoja na changamoto hiyo, Kishaka amesema ufufuaji wa taa hizo unafanyika na zitaanza kufanya kazi muda si mrefu, kisha Tarura ianze kufunga taa zingine mpya katika mitaa mbalimbali. “Tumeshatambua namna ya kudhibiti wizi huo, kazi inaendelea. Kadhalia suala la kurudishia alama za barabarani nalo tunaendelea nalo ,” amesema.

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button