“Ongezeni jitihada kuwafikia wafanyabiashara wadogo”

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), imeagizwa kuwafikia wafanyabiashara ambao hawajarasimishwa ili kusajili biashara zao kwa lengo la kukuza sekta ya uchumi hapa nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba ametoa maagizo hayo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila katika maonesho ya kwanza ya Brela na wadau yaliyofanyika viwanja vya Mlimani City.

“Brela ongezeni jitihada za kuwafikia wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati ambao hawajarasimishwa ili wasajili biashara zao ili kukuza sekta ya uchumi kwa ujumla,” amesema.

Amesema Mkoa wa Dar es Salaam umejaa wafanyabiasara wakubwa, wa kati na wadogo moja ya wajibu wa Brela ni kuhakikisha wafanyabiashara hao wanakua kwa kuwa serikali inalenga kukuza sekta ya uchumi.

Amesema ili serikali ikuze sekta hiyo ya uchumi ni lazima iwe na watu ambao wamerasimishwa, na urasimishaji huo unaanza na Brela.

“Endeleeni kutumia vyema maonesho hayo ili kuimarisha mahusiano na wadau kwa kufikia taasisi zote ambazo zinapaswa kufanya kazi kwa karibu na Brela.

“Yawezekana wananchi wakawa tayari kurasimisha biashara zao, kufungua kampuni na kusajili lakini ili wafikie hapo lazima Brela ifanye kazi kwa karibu na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambao ni muhimu,” amesema.

Ametaka wakala huo kutumia maonesho hayo ya siku tano kuwakutanisha wadau hao pamoja na taasisi ya Nida ambayo wananchi wamekuwa wakiikimbilia kupata namba za utambulisho zinazowafungulia mlango kwenda Brela kufanyiwa usajili na kurasimisha shughuli zao.

Pia aliwataka wakala huo kuangalia namna ambayo watakuwa na madawati ya pamoja ya kimtandao katika utoaji wa huduma zao.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu Brela, Godfrey Nyaisa amesema maonesho hayo yamefungua njia kwa kuwa wakala huo itaendelea nayo katika maeneo mengine hapa nchini ili kukutana na wajasiriamali kwa ukaribu.

Amesema kupitia maonesho hayo wananchi wataelewa juu ya upatikanaji wa huduma zinazochangia ukuaji na ustawi wa biashara na sekta ya viwanda nchini, ikiwa ni pamoja na huduma saidizi zitolewazo na taasisi mbalimbali.

Amesema taasisi 11 zimeshirikia katika maonesho hayo ambayo lengo lake ni kuimarisha uhusiano na mawasiliano baina ya brela na wadau wake ili kujenga uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na wakala huo pamoja na kupata mrejesho kuhusu ubora wa huduma hizo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button