Papa Francis afariki Dunia akiwa na miaka 88

VATICAN – Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, amefariki dunia leo asubuhi akiwa na umri wa miaka 88. Taarifa rasmi kutoka Vatican zinasema alifariki saa 1:35 asubuhi kwa saa za huko, katika makazi yake ya Casa Santa Marta, baada ya kuugua kwa muda mrefu kutokana na nimonia ya mapafu yote mawili.
Papa Francis, ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio, alizaliwa mwaka 1936 jijini Buenos Aires, Argentina. Alikuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika Kusini na pia Papa wa kwanza kutoka shirika la Jesuit, akichaguliwa mwaka 2013.
Utawala wake ulitambuliwa kwa msisitizo wake juu ya unyoofu, haki za kijamii, huduma kwa wanyonge, na mageuzi ndani ya Kanisa Katoliki. Alijitahidi pia kuhimiza usawa wa kijinsia, utunzaji wa mazingira, na uwazi katika kushughulikia kashfa za unyanyasaji wa kingono ndani ya Kanisa.
Kwa mujibu wa matakwa yake ya kibinafsi, Papa Francis atazikwa katika Kanisa Kuu la Santa Maria Maggiore mjini Roma, ndani ya jeneza la mbao rahisi, badala ya maziko ya kifalme chini ya Kanisa la Mtakatifu Petro.
Mazishi yanatarajiwa kuvuta maelfu ya waumini kutoka duniani kote, huku viongozi wa kidini na wa kisiasa wakitoa salamu za rambirambi na kutambua mchango wake mkubwa kwa dunia.