TPBA yawataka TLS kuzingatia maadili ya uwakili

DAR ES SALAAM: CHAMA cha Mawakili wa Serikali (PBA) kimepinga vikali hatua ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutoa maelekezo yanayozuia wanasheria kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, kufuatia tukio la kushambuliwa kwa Wakili Deogratius Mahinyila na askari polisi Septemba 15, 2025, alipokuwa akifuatilia kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 23, 2025, Mwenyekiti wa PBA, Addo Mwasongwe, amesema kutokana na matamko na maazimio mbalimbali yaliyotolewa na TLS yaliyolenga kuzuia mawakili kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi ni kinyume na misingi ya taluma ya uwakili na pia ni uvunjaji wa haki za kikatiba za wananchi kupata msaada huyo
“Jukumu mojawapo la wakili ni lazima uwe unatoa msaada wa kisheria, kuna watu wenye uwezo na kuna watu wasio na uwezo. Kwa wasio na uwezo tumelazimishwa na sheria kwamba ni lazima kuwahudumia na sio suala la maamuzi yetu sisi” amesema Mwasongwe.
SOMA ZAIDI
Ameeleza kuwa TLS haina mamlaka yoyote ya kuzuia misaada ya kisheria, na kwamba hatua hiyo inahatarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wa kawaida. “Kitendo cha TLS kinavuruga mfumo wa utoaji haki na kinawanyima wananchi haki yao ya kikatiba,” amesisitiza.
Akirejea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwasongwe amesema Ibara ya 26(1) inaweka wazi kuwa kila mtu ana wajibu wa kufuata na kuitii Katiba pamoja na sheria za nchi. Hivyo, ni kinyume cha Katiba kwa TLS kuzuia wanachama wake kutoa huduma ya kisheria kwa wananchi “TLS wanapata wapi uhalali wa kuwaambia wanachama wao wasitoe msaada wa kisheria wakati huo ni wajibu wa kisheria na kikatiba?” amehoji Mwasongwe.
Aidha, Mwasongwe ameutaarifu Umma kuwa TLS wamekosea, wamevunja sheria na pia hawana mamlaka ya kuzuia misaada ya kisheria isitolewe, na wanadanganya Umma kwasababu mwenye mamlaka ya kutunga sheria kwa mujibu wa Katiba ni Bunge pekee.
Hata hivyo, Mwasongwe ametoa wito kwa wanasheria wote nchini kuendelea kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia sheria na Katiba, huku akisisitiza kuwa kutoa msaada wa kisheria si hisani bali ni wajibu wa kitaaluma.