Pinda atoa maagizo matumizi ya ardhi

KATAVI: Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amewaasa watanzania kuhakikisha wanakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo kwa kuwa ardhi iliyopo haiongezeki na idadi ya watu inazidi kuongezeka.

Pinda amesema hayo Desemba 26, 2023 nyumbani kwake Kibaoni, Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi katika hafla maalum ya chakula aliyowaandalia wananchi na viongozi wa jimbo lake kusheherekea Sikukuu ya Christimas.

Advertisement

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, alisema, wakati serikali ikiandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, watanzania wanatakiwa kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi huku wakielewa changamoto kubwa iliyo mbele yao ni kuwa ardhi haiongezeki.

‘’Miaka 25 inayokuja lazima tufikirie hizi hekta na ekari tulizopopewa na Mungu ikaitwa Tanzania inatoshaje itakapofika miaka hamsini ijayo, kwa hiyo ni sisi ndiyo tutakaopanga tutumiaje maeneo yetu’’ alisema Pinda.

‘’Kila mtu akikaa ajue ardhi ni yake na ndugu zake kwa hiyo tuishi kwa amani na tusigombane, hakuna namna tutakachokifanya katika eneo hili ni lazima tukubaliane namna ya kuitumia ardhi ndogo katika ongezeko kubwa la watu’’. Alisema Pinda.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amemtaka Mbunge wa Jimbo la Kavuu ambaye ni mdogo wake kuwa karibu na wananchi  wakati wote wa juhudi mbalimbali za kuliletea maendeleo jimbo lake.

‘’Hoja kubwa ya wananchi unaowaoongoza ni mahusiano, mnaishije? kila aliyesimama amekupa sifa ni jambo zuri kazi yako sasa ni kutoharibu sifa, kaza uzi na jishushe kadri inavyowezekana na watu wote ni wa kwako hata wale mliopingana’’ alisema Mizengo Pinda.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda yuko jimboni kwake katika Halmashauri ya Mbimbwe Mkoa wa Katavi kujumuika wananchi wa jimbo la Kavuu pamoja na mambo mengine kusheherekea Sikukuu ya Christimas na wananchi wa jimbo lake.

15 comments

Comments are closed.