Polisi Mtwara: Wanahabari mko salama uchaguzi

MTWARA: JESHI la Polisi mkoani Mtwara limewahakikishia usalama na amani waandishi wa habari mkoani humo wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

Hayo yamejiri leo Septemba 20,2025 wakati wa mdahalo kuhusu usalama kwa waandishi wa habari Mkoa wa Mtwara kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025 uliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Mdahalo huo umeandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC) chini ya UTPC na kukutanisha wadau mbalimbali mkoani humo likiwemo jeshi hilo na wadau wengine ambapo mada mbalimbali zimetolewa ikiwemo usalama kwa wanahabari kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba.

Akizungumza alipofungua mdahalo huo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, SACP Issa Sulemani amesema moja ya jukumu la jeshi hilo ni kulinda usalama wa waandishi na vitendea kazi vyao pamoja na watu waliyoko eneo la tukio husika.

“Sisi jeshi la polisi hatuna wasi wasi na ninyi tuendelee kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na niwasihi tu kutoa habari zenye tija na tuendelee na utamaduni wetu wa kuhabarisha au kuwalisha wananchi habari zenye tija,”amesema Issa.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Mtwara Thimotheus Sullusi amezungumzia suala la haki na wajibu wa wanahabari ikiwemo kulinda vyanzo yake vya habari, kutekeleza majukumu yake bila kubaguliwa na mengine.

Mwakilishi kutoka Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani humo, Baltazar Komba ameawaomba wanahabari hao kuelekea uchaguzi huo wahakikishe wanatoa taarifa zenye tija kwa taifa ili kuufanya uchaguzi ujao kuwa wenye tija zaidi.

Mwenyekiti wa MTPC Grace Kasembe amesema lengo la mdahalo ni kuimarisha ushirikiano kati ya wanahabari, jeshi la polisi na wadau wengine mkoani humo.

Katibu wa MTPC Bryson Mshana amewasisitiza wanahabari hao kuendelea kusimamia maadili ya taaluma hiyo pia amevitaka vyombo vya habari husika kuwatafutia waandishi wao kitu cha utambulisho wakati wanapotekeleza majukumu hayo ikiwemo makoti.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button