JESHI la Polisi kwa kushirikiana na Kampuni ya Mtandao wa Simu wa Vodacom wametoa elimu kwa jamii namna utapeli wa mitandaoni unavyofanyika na nini kifanyike ili kuepukana na wizi huo wa kimtandao.
Hayo yameelezwa Desemba 5,mwaka huu katika mahojiano yaliyofanyika na maofisa wa jeshi la polisi na vodacom Dar es salaam lengo likiwa ni kuongeza uelewa kwa wananchi na watumiaji wa mitandao ili kupunguza matukio ya utapeli ya mtandaoni.
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Waziri Makang’ila alifafanua kuwa wizi wa aina hiyo unaweza kufanyika kwa kutumia matangazo ya ofa za vitu yanayojitokeza wakati wa kutumia programu mbalimbali yakiwa na lengo la kukushawishi uvutiwe na ofa na zawadi unazokuwa ukipewa.
Alisema kuna matangazo ambayo ni halali na mengine ni kwa ajili ya kufatilia shughuli unazofanya katika simu wakishajua nini kinafanyika wanatuma ujumbe mfupi kwa ajili ya kukushawishi.
“Mtu anaangalia tabia ya simu yako na shughuli unazofanya unakuta unacheza sana michezo ya bahati nasibu wanaona waende na njia hiyo wanakutumia ujumbe kwamba umeshinda milioni 100 na wanakupa namba ya kuwasiliana ili uweze kupata na wanakwambia ili kupata fedha hiyo unatakiwa utoe kiasi kadhaa ili uweze kupata,” alisema Makang’ila.
Pia alisema njia nyingine ni kutumia njia ya kutafuta wachumba mitandaoni kwa watu wanaodhani wanaweza kutoka kimaisha kwa kupata wapenzi wanaotoka nchi za mbali anapakua programu inayomuelekeza kuwa anaweza kupata wachumba.
Alisema wengi wa watumiaji wa programu hizo bila kujua anaweza kuwa anaweka taarifa zake bila yeye kujua na kujikuta anatapeliwa kutokana na imani aliyojijengea kwa mtu aliyedhani yupo naye kimapenzi.
Makang’ila alisema njia nyingine ni kupitia ujumbe mrefu unaotumwa kwenye barua pepe wa mtu kujifanya anahitaji msaada, na watu kusajiliwa laini za simu na watu wengine kutokana na kutokujua kusoma na kuandika wanakuja kuibiwa kwa sababu wanajua nywila zao.
Ofisa wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom, Shamte Mikumuo alisema takwimu ya walalamikaji imepungua ukilinganisha na siku za nyuma kutokana na elimu iliyokuwa ikitolewa na mitandao ya simu, polisi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa wananchi.
Aidha Mikumuo alisema namba inayotumika kwa ajili ya huduma kwa wateja ni 100 tu na kuwataka watu kutokubali kupigiwa na namba tofauti na hiyo wakidai ni huduma kwa wateja pia aliwataka kutoa taarifa mapema baada ya kupoteza laini ili kusaidia kuhifadhi taarifa zako.
Pia alieleza namna wanayotumia katika kurudisha miamala ilitotumwa kimakosa alisema miamala huwa inarudishwa ikiwa tu imethibitika kweli ilituma kimakosa na kuwa hawa huduma ya kushikilia muamala uliotolewa baada ya kutumwa kimakosa.
“Ikiwa pesa ilitumwa kimakosa kuna huduma ya jihudumie unaweza kuzuia muamala na vodacom tukapiga simu kwa aliyetumiwa kimakosa ili kuthibitisha ilitumwa kimakosa kama hatujafika muafaka tutaoiga simu ya mkutano tuone nani anasema ukweli,” alisema Mikumuo.
Mtaalamu wa Uchunguzi na Udanganyifu wa Kiforensiki, Rona Katuma alisema wamelenga kuelimisha watu ili waweze kujua na kuongeza umakini kuwa ni njia zipi zinatumika kufanya utapeli wa mitandaoni na kutaja namba ya 15040 kwa kutoa taarifa Vodacom ikiwa umetapeliwa.
Mratibu Msaidizi wa Polisi, Beatrice Charles alisema ili kuepukana na utapeli wa mitandaoni watu wanatakiwa kuacha kutoa taarifa zao binafsi, kutojihudisha kwenye mawasiliano na watu wasioaminika, wakupige simu huduma kwa wateja kwa uthibitisho wa tarifa za miamala.
“Kuna wananchi wengine wanatoa taarifa za nywila zao kwa ndugu zao na familia , wengine wanarithisha kabisa wakati kiusalama sio sawa huwezi huwezi kumuamini mtu mwenye nywila yako anaweza kukuibia fedha,” alisema Beatrice.