Polisi yaanza oparesheni watoto wa mitaani Geita

JESHI la Polisi mkoani Geita limefanikiwa kuwarejesha makwao jumla ya watoto 19 wa mtaani na wasio na makazi maalum ikiwa ni sehemu ya oparesheni maalumu ya kupunguza wimbi la watoto wa mtaani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo ametoa taarifa hiyo katika semina ya polisi jamii kwa watendaji wa kata, wenyeviti wa vijiji na maofisa tarafa.
SACP Jongo amesema takwimu hizo ni mpaka Machi 18, 2025 tangu kuanza kwa oparesheni hiyo iliyodhamiria kukabiliana na ongezeko la watoto wa mitaani mjini Geita ambalo limebainika kukua kwa kasi.
Amesema jeshi la polisi limeamua kuja na mbinu mbadala ya kufanikisha oparesheni hiyo kwa kuhusisha jamii kwa ukaribu kutokana na njia tofauti wanazotumia watoto hao kusafiri na kuishi nje ya familia zao.
“Watoto hawa tumeendelea kuwakamata kidogo kidogo tu, unajifanya kama unataka kumsaidia ukimaliza unamshika unamhoji anakuelekeza kwao ni wapi”, amesema SACP Jongo.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini sababu kubwa ya ongezeko la watoto wa mtaani mjini Geita ni malezi dhaifu ya wazazi wengi kutojali na hata kutofuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao.
“Watoto wanaingia kwenye mabasi, wengine wanapanda kwenye malori, wanapopakia mizigo kabla hawajafunga na wao wanaingia, kwa hiyo wamekuwa na mbinu mbalimbali za kusafiri”, amesema SACP Jongo.
Amesema oparesheni hiyo ni endelevu, ambapo jeshi la polisi linaendelea kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa pamoja na polisi jamii kufanikisha oparesheni hiyo.
“Nitoe wito kwa wazazi tuwajue watoto wetu, haiingii akilini mzazi amepoteza mtoto ana miezi mitatu, miezi sita na hata mwaka mmoja hujui mtoto alipo na unaishi tu na maisha yanaendelea.
“Tunao wajibu kwa hawa watoto kama siyo duniani basi kwa Mungu atatuuliza kwa nini hawa watoto tuliwaleta duniani harafu tukashindwa kuwapa malezi bora”, amesisitiza SACP Jong



